Kitaifa

MADAKTARI WA UPASUAJI WA MASIKIO WA HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKO ANA NA KANDA WAJENGEWA UWEZO MUHIMBILI

Written by mzalendo

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Hearwell Audiology Clinic zimeendesha mafunzo ya siku tatu kwa wataalam kutoka hospitali mbalimbali nchini yenye lengo la kuwajengea uwezo juu ya upasuaji wa masikio.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa MNH, Dkt. Rachel Mhavile amesema kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa madaktari kutoka hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini ambapo yatahusisha njia ya nadharia na vitendo.

“Mafunzo haya yatakuwa endelevu hivyo tutapata matokeo chanya kwakuwa yatakuwa kuwa baada ya hapa mtakuwa mmeongeza ujuzi zaidi kwenye eneo la upasuaji wa masikio na mtapata fursa ya kuingia katika vyumba vya vyetu vya upasuaji kuona namna ambavyo huduma za upasuaji zinavyofanyika,” amesema Dkt. Mhavile

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Masikio, Pua na Koo Dkt. Aslam Nkya amesema kuwa mafunzo hayo ni muendelezo wa Hospitali ya Muhimbili kuwajengea uwezo wataalam wa ngazi za mbalimbali ili kuhakikisha kuwa huduma za kibingwa na bobezi za upasuaji wa masikio zinawafikia wananchi wengi zaidi.

Watalaam hawa wametoka Hospitali ya Bugando, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Agakhan, Lugalo, Tumbi, Temeke na Mnazi Mmoja.

About the author

mzalendo