Featured Kitaifa

MTATURU AWASEMEA WAFUGAJI.

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu(CCM),ameihoji serikali ni lini itajenga majosho kwenye vijiji vya Jimbo la Singida Mashariki ili kulinda afya za mifugo.

Mtaturu ameuliza swali hilo Februari 12,2024,Bungeni Jijini Dodoma.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote zilizotengewa fedha za ujenzi wa majosho kuwasilisha nyaraka za maombi ya fedha hizo mapema Wizara ya Fedha ili waweze kupatiwa.

Amesema Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa majosho nchini ili kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na kupe na wadudu wengine ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Sekta ya Mifugo imetenga jumla ya shilingi bilioni 5.7 kwa ajili ya ujenzi wa majosho 246 katika Halmashauri 63 nchini.

“Katika Jimbo la Singida Mashariki mwaka 2022/2023 Serikali ilijenga majosho manne ambayo ujenzi wake ulikamilika na yanafanya kazi,”amesema.

Pia, katika mwaka 2023/2024, majosho manne yanajengwa katika vijiji vya Ndughamunga, Unyampanda, Ughandi na Ngamu vilivyopo katika Kata za Mughunga, Ughandi na Mwasauya.

Mnyeti ametoa wito kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote zilizotengewa fedha za ujenzi wa majosho kuwasilisha nyaraka za maombi ya fedha hizo Wizara ya Fedha mapema kama walivyoelekezwa ili waweze kupatiwa fedha hizi za ujenzi wa majosho.

Katika swali la nyongeza, lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Aysharose Matembe kwa niaba ya Mbunge Mtaturu , amesema kwa kuwa serikali katika mwaka huu wa fedha iliahidi kujenga majosho katika vijiji vya Siuyu, Ulyampiti, Isuna na Msule lakini hadi sasa hayajajengwa na hata tenda haijatangazwa, lini mchakato huo utafanyika.

Aidha, amesema kwa kuwa wananchi wa Singida ni wafugaji wazuri wa mifugo ya aina mbalimbali lakini hawana elimu ya kutosha kuhusu ufugaji, nini mkakati wa serikali wa kutoa elimu bora ili kuongeza mazao ya ufugaji kwa wananchi.

Akijibu maswali hayo, Mnyeti amesisitiza kuwa wizara imeshatoa maelekezo kwa wakurugenzi wote nchini ambao walitengewa bajeti ya ujenzi wa majosho ambapo fedha zipo tayari wanachotakiwa ni kupeleka maombi ili wapatiwe.

“Nawaomba wabunge wanapokuwa kwenye vikao vya kamati za fedha na mipango kwenye halmashauri wawe wakali kuwasukuma wakurugenzi kuomba hizi fedha maana yake baadhi ya wakurugenzi ni wavivu wanashindwa kuziomba hizi fedha zipo tayari , wengine tayari lakini wae wavivu ndio bado hali inayosababisha kuwa na mrundikano mwingi wa fedha kwenye halmashauri”amesema.

Kuhusu utoaji elimu kwa wafugaji amesema wizara imeshaanza kutoa elimu juu ya ufugaji bora, wa kisasa na kuachana ufugaji wa zamani wa kufuga ng’ombe wengi wasio na tija na hilo limeshafanyika mikoa mbalimbali.

About the author

mzalendoeditor