Zaidi ya Wakazi 2000 katika Mitaa miwili ya Maporomoko na Kiwanja cha ndege, Kata ya Nzega Mjini Mashariki Wilayani Nzega, wamejitokeza kuhakiki taarifa zao za umiliki ili kubaini kama kuna makossa yoyote au mapungufu wakati wa zoezi la ukusanyaji wa taarifa hizo kabla ya umilikishwaji wa vipande vyao vya Ardhi.

Akizungumza na Afisa wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa milki za ardhi (LTIP) Mwenyekiti wa Mtaa wa Maporomoko uliopo Kata ya Nzega Mjini Mashariki Bi. Zuhura Salum amesema zoezi la uhakiki litawasaidia wananchi kupata nafasi ya pili ya kurekebisha katika maeneo ambayo walikosea kutoa taarifa zao za umiliki kama vile namba za simu, NIDA, mipaka pamoja na majina yao.

Pia amesema kuwa wakati zoezi likiendelea wamekua wakisuluhisha migogoro midogomidogo ya umiliki hasa ya kifamilia katika maeneo ambayo mwenza mmoja alijimilikisha pekeyake bila kumshirikisha mwingine na wamekua wakiwasaidia kufikia muafaka wa kumiliki pamoja kwa hiyari yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Kiwanja cha ndege Bi. Suzana Bakaza amesema kuwa faida kubwa ya kuhakiki taarifa za umiliki ni kuondoa migogoro na migongano baina ya wananchi na kuwasaidia kujua ukubwa wa maeneo yao na mipaka jambo ambalo hapo nyuma liliwaletea sinto fahamu kubwa.

Bi. Bakaza ameongeza kuwa wataendelea kuwahamasisha wananchi Zaidi waweze kujitokeza kwenye zoezi hilo ambalo litadumu kwa wiki mbili kwani linafanyika kwa manufaa yao na linawapa nafasi ya kusahihisha pale ambapo walikosea jambo ambalo manufaa yake watayaona wakati wa umilikishwaji.

Aidha Bw. Patrick Magilibanya ambae ni Mkazi wa Mtaa wa Maporomoko ameushukuru Mradi wa LTIP kwa kuendesha zoezi hilo kwa uwazi na usawa ili kila mwananchi aweze kuona taarifa zake hadharani kwani kwa kufanya hivyo kunawabainisha hata wale ambao hawakua wamiliki halali wa maeneo na kuwatolea taarifa ili kuwapata wamilki halali wa maeneo hayo.

“Wapo watu wangeweza kujimilisha maeneo yasiyo yao kwa kigezo cha wahusika kutokuwepo ila zoezi hili litawabaini na kusaidia kuwapata wahusika” aliongeza Bw. Magilibanya.

Zoezi la uhakiki wa taarifa za awali za umilki (Public display) lilianza tarehe. 5/2/2024 katika Mitaa miwili ya Maporomoko na Kiwanja chandege na linatarajiwa kuendele kwa wiki mbili huku Zaidi ya vipande vya ardhi 4492 vikitarajiwa kuhakikiwa katika Mitaa hiyo hilo.

Previous articleBILIONI 9 ZA CSR KUTOKA BARRICK NORTH MARA KUTUMIKA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO YA WANANCHI WILAYANI TARIME
Next articleUJENZI WA NYUMBA ZA WAATHIRIKA WA MAAFA HANANG’ UZINGATIE UBORA NA THAMANI YA FEDHA-WAZIRI MHAGAMA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here