Na Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Ummy Nderiananga amesema Serikali inahitaji taasisi zake kuongeza ufanisi na tija katika utendaji wake ili kuongeza kasi ya maendeleo katika kukuza uchumi wa watanzania na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya saba ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Jijini Dar es Salaam na kuitaka bodi hiyo kuwa wabunifu huku wakifanya kazi kwa uadilifu na weledi ili kuchochea ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi nchini.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais shupavu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imewaamini hivyo ni jukumu lenu sasa kuonesha mchango wenu ikiwa ni pamoja na kusimamia utendaji wa Baraza. Naamini kwa umoja wenu na ushirikiano na Menejimenti ya (NEEC) mtaweza kufanikisha hili na kuleta matokeo chanya katika kukuza uchumi wa Taifa,”Alisema Mhe. Ummy.
Mhe. Ummy amelikumbusha kwamba Mafanikio ya (NEEC) yanategemea kwa kiasi kikubwa miongozo na utendaji wa Bodi kuibua na kubuni mbinu zitakazoweza kuongeza wigo wa utoaji huduma za uwezeshaji kwa weledi na kufikia wananchi wengi.
“Bodi hii inatarajiwa kutekeleza majukumu yake kwa kipindi cha miaka mitatu, hivyo ni jukumu la Bodi kuhakikisha kuwa, Baraza linafikia malengo na matarajio ya wananchi katika kipindi chote cha utendaji wake,”Alisisitiza.
Aidha, aliielekeza Menejimenti ya (NEEC) kuhakikisha kuwa inapokea na kutekeleza maagizo na maelekezo yote yatakayotolewa na Bodi hiyo kwa lengo la kuboresha ufanisi katika kuimarisha utoaji huduma za uwezeshaji.
Awali akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika ofisi hiyo Bi. Stella Mwaiswaga alibainisha kuwa baraza hilo lina jukumu la kuhakikisha linasimamia utekelezaji wa sera ya Taifa ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi.
“Tunatambua umuhimu wa Baraza hili la Saba katika kuiongoza na kuisimamia (NEEC) kuhakikisha inafanya majukumu yake ipasavyo kwa ajili ya wananchi. Pia niwapongeze wajumbe wapya pamoja na wanaomaliza muda wao kwa kazi nzuri waliofanya katika baraza la sita,”Alibainisha Bi. Stella.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng’i Issa, aliahidi kwamba menejimenti ya (NEEC) kwa kushirikiana na wadau watafanya kazi kwa karibu na bodi hiyo ili kufikia azma ya Serikali ya kukuza ushiriki wa watanzania katika shughuli za kiuchumi yakiwemo makundi maalum wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.
Naye Mjumbe wa Bodi aliyemaliza muda wake Prof.Lucian Msambichaka alisisitiza kuwa ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia Sera, Sheria na Kanuni haina budi kufanya kazi kwa umoja na kujitoa.
“Katika kufanikisha azma ya Serikali ya kuwafanya wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi mkiwa kama wasimamizi na washauri wa Baraza kuna kila sababu ya kufanya kazi kwa umoja na kushirikiana na wadau mbalimbali katika mnyororo wa uwezeshaji,” alisisitiza Prof. Msimbachaka.