Featured Kitaifa

DKT.MPANGO  AWEKA JIWE LA MSINGI SHULE YA WASICHANA YA SAMIA SULUHU LONGIDO

Written by mzalendo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiweka jiwe la msingi Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Samia Suluhu iliyopo Wilaya ya Longido mkoani Arusha. Tarehe 10 Februari 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Longido mara baada ya kuweka jiwe la msingi Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Samia Suluhu akiwa ziarani mkoani Arusha tarehe 10 Februari 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwaaga wananchi wa Longido mara baada ya kuweka jiwe la msingi Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Samia Suluhu akiwa ziarani mkoani Arusha tarehe 10 Februari 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa eneo la Oldonyohasi Wilaya ya Longido wakati akiwa ziarani mkoani Arusha tarehe 10 Februari 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameutaka uongozi wa Wilaya ya Longido na Mkoa wa Arusha kuhakikisha Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Samia Suluhu inakamilika ndani ya muda wa nyongeza uliokubaliwa yaani tarehe 28 Machi, 2024. 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Samia Suluhu iliyopo Wilaya ya Longido mkoani Arusha. Ameitaka TAMISEMI kufanya ukadiriaji wa gharama za ujenzi wa uzio na kushirikiana na wadau wa Mkoa ili kuhakikisha ujenzi wa uzio na nyumba za watumishi unaanza kutekelezwa. Ameongeza kwamba kukosekana kwa uzio na nyumba za watumishi kunaweza  kuhatarisha usalama wa wanafunzi kutokana na eneo hilo kuwa ni ushoroba wa wanyama pori. 

Pia Makamu wa Rais ameielekeza TAMISEMI kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa, wananchi wa Longido na wadau kwa mwaka ujao wa fedha kupanga kuongeza idadi ya shule za sekondari katika wilaya ya Longido  ili kuhakikisha watoto wa wilaya hiyo wanaoandikishwa wanaendelea na masomo ya Sekondari. Amesema msukumo zaidi unahitajika katika ujenzi wa shule za bweni, kwa kuzingatia mazingira ya jamii ya wafugaji iliyopo eneo hilo. 

Makamu wa Rais amesema idadi ya wanafunzi wanaoripoti shuleni katika Wilaya ya Longido hairidhishi ambapo wanafunzi walioripoti Kidato cha Kwanza kwa mwaka 2024 ni asilimia 49.2 tu ya wanafunzi 2,147 waliochakuliwa kujiunga Kidato cha Kwanza. amewahimiza Watendaji wote wa Serikali, Wazazi, na jamii nzima kushirikiana kupambana na changamoto zinazokwamisha jitihada za Serikali katika kuboresha elimu ikiwa ni pamoja na kupiga vita mimba zinazotokana na ndoa za utotoni.

Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha maji kutoka chanzo cha Kisima kilichopo Kata ya Sinya yanafika katika mji wa Namanga mapema ili kuwaondolea adha wanayopata wananchi wa eneo hilo.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amezungumza na wananchi wa eneo la Oldonyohasi akiwa ziarani mkoani Arusha. 

Makamu wa Rais amekemea tabia ya askari wa SUMA JKT kuchukua hatua mkononi ikiwemo kuwapiga raia wa eneo hilo wanaotumia msitu uliopo kijijini hapo. Amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Kamishna wa Wakala wa Misitu (TFS) kuhakikisha wanakutana na kumaliza mgogoro huo. Pia ameitaka TAMISEMI kushughulikia changamoto ya soko kwa kujenga soko litakalokidhi mahitaji ya wananchi wa Oldonyohasi.

About the author

mzalendo