Featured Kitaifa

KINANA AITAKA CHADEMA KUTHAMINI NIA NJEMA YA RAIS SAMIA KATIKA MARIDHIANO.

Written by mzalendoeditor

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana, amesema nia njema iliyooneshwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutaka maridhiano inapaswa kuendelezwa na vyama vyote vya siasa.

Aidha, amevishauri vyama vya siasa vya upinzani hususan CHADEMA kuacha kufanya maandamano yasiyo na msingi badala yake wathamini utayari wa Dk. Samia katika kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa katika maendeleo yakiwemo ya demokrasia.

Kinana ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, ambapo alitumia muda mwingi kuzungumzia, maridhiano yaliyoingiwa kati ya CCM, CHADEMA na vyama vingine vya upinzani nchini.

Kinana aliitaka CHADEMA kueleza ukweli kuhusu mambo mazuri yaliyopatikana baada ya kuwepo kwa maridhiano ikiwemo serikali kukipatia chama hicho ruzuku ya Sh. bilioni 2.7 ambayo waliikataa kwa miaka mitatu nyuma.

Akielezea kuhusu sheria mpya, Kinana alisema pamoja na uzuri wake ikiwemo kuzingatia maoni ya wadau wakiwemo CHADEMA wenyewe, lakini bado kinasema haifai.

“Nilifikiri sheria hii mpya wangesema itatufikisha mbali zaidi, lakini wao wanasema hii haifai, basi turudi kule. Sheria ya sasa ni bora kwa muundo, kwa maudhui, kwa malengo, kwa dhamira sijui mnanielewa?. Nitumie nafasi hii kuwasihi ndugu zangu wa CHADEMA waungane na Watanzania waachane na mandamano, waangalie dhamira ya Rais.

“Hivi Rais na baraza lake la mawaziri kama wasingepeleka hii sheria mpya ya uchaguzi nani angemlazimisha? Lakini Rais busara imemuongoza akasema hapana hebu twende pamoja na mimi ndio mtetezi mkubwa wa maridhiano na ustahimilivu. Hebu tupeleke sheria mpya bungeni na kila hoja aliyopelekewa, aliyoambiwa kwamba haya ndio maoni ya wadau Rais akasema sawa, nakubali,” amesema.

About the author

mzalendoeditor