NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa maji katika vijiji 57 Wilayani Kyerwa.
Amesema hadi sasa, utekelezaji wa mradi huo unaendelea katika vijiji 27 ambavyo ni Nkwenda, Rwabwere, Karongo, Nyamiaga, Nyakatera, Kagu, Masheshe, Nyamweza, Kaikoti, Iteera, Muleba, Chanya, Kimuli, Rwanyango, Chakalisa, Kikukuru, Omukitembe, Karambi, Rwele, Rubilizi, Mukunyu, Kitwechenkura, Rukuraijo, Makazi, Kibimba, Nyakatete na Mabira.
Mhandisi Mahundi ameyasema hayo leo Januari 30, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Kyerwa Innocent Bilakwate aliyetaka kufahamu lini Mradi wa maji wa Vijiji 57 ambao utaanzia Kyerwa, Nyakatuntu mpaka Kamuli Wilayani Kyerwa utaanza ili Wananchi wapate maji.
Mhandisi Mahundi amesema kazi zinazotekelezwa katika miradi hiyo ni pamoja na ujenzi Matenki Matano (5) yenye jumla ya ujazo wa lita 1,450,000, ulazaji wa mabomba umbali wa Kilometa 110, ujenzi wa Vituo 102 na Vioski 18.
Amesema Utekelezaji wa miradi hiyo umefikia wastani wa asilimia 80 na inatarajiwa kukamilika Mwezi Mei, 2024 na kuwanufaisha wananchi wapatao 83,000. Miradi katika Vijiji 30 vilivyobaki itatekelezwa katika mwaka wa fedha 2024/25.