Kitaifa

MRADI WA EPIC WAWAJENGEA UWEZO WABUNGE

Written by mzalendo

Na Mwandishi wetu- Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imejengewa uwezo kuhusu Mpango wa DREAMS unaotekelezwa na Mradi wa EPIC ambapo mpango huo unalenga katika kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU miongoni mwa wasichana balehe na wanawake vijana.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango huo katika semina ya Kamati hiyo Bungeni Jijini Dodoma Mratibu wa Mpango wa DREAMS Mkoa wa Shinyanga Bi. Agness Tunga amesema Mradi wa EpiC unalenga makundi maalumu na anayohitaji kupewa kipaumbele ikiwemo wasichana wa rika balehe na kina mama vijana, na wanaume na wanawake walio katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU.

Amesema mradi unatekelezwa katika Mikoa 11 Mradi wa EpiC ulianza utekelezaji wa mpango wa DREAMS katika ngazi ya jamii mnamo Februari 2020 kwa Mabinti wa rika balehe (15-19) na Wakina Mama vijana wenye umri kuanzia miaka (20-24).

“Maeneo ya Utekelezaji ni Shinyanga katika Halmashauri za Shinyanga vijijini, Shinyanga mjini, Msalala, Kahama mji na Ushetu kwa upande wa Mkoa wa Iringa ni katika Halmashauri za Mufindi na Iringa mjini, utekelezwaji unafanyika kupitia Asasi za kiraia kwa kushirikiana na serikali na walengwa wa Mpango wa DREAM,”alisema Agness.

Aliongezea kuwa kupitia PEPFAR chini ya USAID wadau mbalimbali wanatekeleza mpango wa DREAMS katika ngazi ya shule, vituo vya Afya na kwenye jamii.

Kupitia Semina hiyo baadhi ya wajumbe wa kamati walitoa maoni yatakayowezesha kuboresha namna ya kutekeleza mpango huo katika jamiii na kuleta matokeo chanya.
Katika hatua nyingine Kamati hiyo ilipokea na kujadili taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu Utekelezaji wa Bajeti ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2023 iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama ambapo wajumbe wa kamati walipta fursa ya kujadili taarifa hiyo.

AWALI
Mpango wa DREAMS ulitangazwa na PEPFAR kwenye siku ya UKIMWI Duniani mwaka 2014. 2015 mpango ulianza utekelezaji rasmi katika nchi kumi zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU kwa ikiwemo Eswatini, Kenya, Lesotho, Malawi, Mozambique, Afrika Kusini, Tanzania, Uganda, Zambia, and Zimbabwe. Mpango wa DREAMS unalenga katika kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU miongoni mwa wasichana balehe na wanawake vijana.

DREAMS (Determined, Resilient, Empowered, AIDS-free, Mentored, and Safe) inaandikwa kama kifupisho chenye maana ya kudhamiria, ustahamilivu, kuwezeshwa, kutokuwa na maambukizi ya VVU, kuongozwa na kuwa salama.

About the author

mzalendo