Featured Kitaifa

PROF. MKENDA ATUMA SALAMU ZA KHERI YA MAADHIMISHO YA SIKU YA ELIMU DUNIANI.

Written by mzalendo
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Maadhimisho ya Siku ya Elimu Duniani kwa Mwaka 2024 yana adhimishwa  wakati Tanzania inaanza safari ya utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 pamoja na mitaala mipya.
Profesa Mkenda akitoa  salamu za kheri ya Maadhimisho ya Siku ya Elimu Duniani asema kuwa baadhi ya mambo muhimu katika Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ni kuanza utaratibu ambao utaongeza muda wa wanafunzi kukaa shuleni kwa lazima kutoka miaka saba mpaka kufika miaka 10.
Kiongozi huyo amesisitiza kuwa katika mwaka huu wa kwanza wa utekelezaji wa sera, mitaala mipya itaanza na wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la kwanza, darasa la tatu, kidato cha kwanza kwa wale ambao wamechukua mkondo wa elimu ya sekondari ya amali, kidato cha tano wanaotarajiwa kuanza katikati ya mwaka huu na mwaka wa kwanza katika vyuo vya ualimu.
“Kwa wale waliopo darasa la tatu Mwaka huu wa 2024 watakapofika darasa la sita watakuwa wamemaliza elimu ya msingi na wataendelea na elimu ya lazima ya miaka minne ili kutimiza miaka 10″ . 
Mkenda amesema mwaka 2027 ni mwaka muhimu kwa mageuzi ya elimu kwani ndio mwaka ambao darasa la sita na la saba watakuwa wanamaliza elimu ya msingi kwa pamoja.
Ameongeza kuwa mageuzi ya elimu yameleta mkondo maalum wa mafunzo ya amali ambapo unaanza kidogo kidogo na inatarajiwa kutakuwa na shule nyingi za sekondari ambazo zinamuandaa mwanafunzi kwa ajili ya mafunzo ya kazi yaani elimu ya ufundi na ufundi stadi ambapo kwa mwaka huu shule za serikali ambazo zimeweza kukidhi kutoa elimu ya amali ni ni 28 na binafsi 68.
Aidha, Prof. Mkenda amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza maagizo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watoto wote wanaotaka kusoma lazima kuhakikisha wanapata elimu, hivyo inaendelea kuwatafuta watoto waliokatisha masomo kwa sababu yoyote kuwapa fursa ya kurudi shule kusoma ili  waweze kutimiza ndoto zao katika mfumo wa elimu rasmi ama elimu mbadala.
Akizungumzia wanafunzi wenye mahitaji maalum. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema kuwa mpaka sasa serikali imeshatumia takribani shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia  kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum na kwamba wale wenye changamoto kubwa serikali imeongeza shule ya sekondari Patandi iliyopo Arusha pamoja na shule ya msingi Lukuledi iliyopo Masasi pamoja na kutoa Miongozo mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa shule ili  kuhakikisha mtoto hapati changamoto za miundombinu na mwongozo wa namna ya kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata huduma ya elimu hata wakiwa nyumbani.

About the author

mzalendo