Featured Kitaifa

WATU 573 WAFIKIWA NA HUDUMA YA TIBA MKOANI TABORA

Written by mzalendo

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani akimkabidhi zawadi za wataalamu wa afya waliofanya kambi ya upimaji wa magonjwa ya moyo mkoani humo Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Parvina Kazahura baada ya kumalizika kwa kambi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita. Wapili kulia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Tabora – KITETE Dkt. Mark Waziri.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani akizungumza na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati akipokea taarifa ya upimaji wa magonjwa ya moyo ujulikanao kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoa uliokuwa ukifanyika mkoani Tabora na kumalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Picha na: JKCI

Na: Mwandishi Maalumu – Tabora 

Watu 573 wamepatiwa huduma ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora –KITETE.

Kambi hiyo iliyofanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 15 Januari imemalizika tarehe 19 Januari 2024 mkoani Tabora ambapo jumla ya watu wazima 531 na watoto 42 walipatiwa matibabu. 

Akitoa taarifa kwa mkuu wa mkoa wa Tabora kuhusu kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Parvina Kazahura alisema wametoa rufaa kwa wagonjwa 84 wakiwemo watoto na watu wazima kufika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwani wanahitaji kupatiwa matibabu zaidi.

Dkt. Parvina alisema upande wa watu wazima wagonjwa wengi wamekutwa na shikikizo la juu la damu, hitilafu katika misuli ya moyo (Ischemic heart disease), pamoja na magonjwa ya valvu za moyo.  

“Upande wa watoto tumekuta watoto wana magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo (Congenital Heart Disease) ikiwemo matundu kwenye moyo na mishipa ya damu ya moyo iliyoziba au kukaa vibaya ambapo tumetoa rufaa kwa watoto tisa kufika JKCI kupatiwa matibabu zaidi”,

“Sehemu zote tunazopeleka huduma ya tiba mkoba idadi ya watoto haiwi kubwa kama ya watu wazima lakini watoto tunaowakuta na shida za moyo tunabadilisha maisha yao kwasababu kuna shida za moyo ambazo watoto wanatakiwa wafanyiwe upasuaji kabla ya kufikisha miezi mitatu, nyingine kabla ya kufikisha mwaka mmoja”, alisema Dkt. Parvina

Dkt. Parvina alisema katika tafiti zilizofanywa kwa wagonjwa waliotibiwa katika kambi hiyo wagonjwa wengi wameonyesha kununua dawa za presha katika maduka ya dawa na kutumia bila ya kufika Hospitali kufanyiwa uchunguzi.

“Tafiti pia zimeonyesha asilimia 60 ya watu wazima waliopatiwa huduma katika kambi hii kuwa na uzito mkubwa, tabia ya kula chakula cha jioni usiku sana na matumizi ya chuvi ya kuongeza juu ya chakula kuwa makubwa sana”, alisema Dkt. Parvina

Akitoa neno la shukrani Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani amewashukuru wataalamu wa afya wa JKCI na kuwaomba kufikisha salamu kwa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo kwa kuwafikishia huduma za matibabu ya moyo.

Mhe. Dkt. Batilda ameomba huduma ya tiba mkoba mkoani Tabora isiishie hapo bali Taasisi ya Moyo ijipange kurejea tena mkoani humo kwani bado wananchi wa Tabora wanawahitaji sana.

“Asanteni sana hasa hapo kwa watoto kwani kama mlivosema kama matibabu ya watoto yatachelewa mtoto anakosa nafasi ya kusaidiwa, kuna dua ya mzazi mmoja mtoto wake kapatiwa matibabu katika kambi hii anawashukuru sana”, alisema Mhe. Dkt. Batilda

Aidha Mhe. Dkt. Batilda amewataka wataalamu wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE kutumia vizuri huduma ya tiba mtandao kuungana na JKCI kuwasaidia wagonjwa wa moyo watakaoendelea kufika katika Hospitali hiyo kupata matibabu.

 

About the author

mzalendo