Mkurugenzi Mtendaji wa AngloGold Ashanti, Alberto Calderon akitembelea mitambo ya uzalishaji dhahabu ya Mgodi wa GGML iliyopo mkoani Geita.
NA MWANDISHI WETU
KUTOKANA na mazingira mazuri ya uwekezaji yanayoendelea kuboreshwa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Kampuni AngloGold Ashanti imetangaza kuanzisha shughuli za utafiti wa madini kupitia kampuni mpya ya Greenfields Mineral Exploration Limited, ikiwa na lengo la kuongeza uzalishaji wa dhahabu nchini ambao sasa unafanywa na Kampuni dada ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa zaidi ya miaka 20 mkoani Geita.
Akizungumzia uwekezaji huo, Mkurugenzi Mtendaji wa AngloGold Ashanti, Alberto Calderon anasema hatua hiyo inalandana na matayarisho ya sherehe za kumbukumbu ya miaka 25 ya uwepo wa GGML nchini Tanzania.
Anaitaja GGML kama mojawapo ya migodi michache ya dhahabu ya daraja la kwanza duniani hivyo, AngloGold Ashanti wanatajia kuiendeleza kampuni hiyo kwa zaidi ya robo karne ijayo na kuifanya kuwa kampuni pekee ya uchimbaji madini.
“Kwa kuzingatia hadhi yake kama mojawapo ya mchimbaji bora wa dhahabu duniani, ni wazi tungependa kuongeza uwepo wetu hapa Tanzania na viwango vya uzalishaji nchini ndiyo maana tunafanya uwekezaji huu kutafuta hifadhi nyingine ya dhahabu ya kiwango cha kimataifa nchini Tanzania.”
AngloGold Ashanti, mzalishaji wa nne kwa ukubwa wa dhahabu duniani, ni kampuni yenye mojawapo ya programu za kimataifa za utafutaji wa dhahabu ambazo mbali na Tanzania zinatekeleza majukumu hayo ya uvumbuzi pia katika nchi za Australia, Marekani na Kolombia.
Kuanzishwa kwa ofisi mpya kampuni hii ya Greenfield Exploration ambayo ni mahususi ya uchunguzi wa maeneo ya mjini Dodoma, kutasaidia kuelekeza utaalamu na rasilimali zake katika miradi mitatu tofauti ya utafiti itakayotekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga na Singida ambapo kampuni inaamini kuna uwezekano wa kupata hifadhi ya dhahabu sawa na hii ya GGML inayotambulika duniani.
GGML, ambayo ilizalisha wakia yake ya kwanza ya dhahabu mnamo Juni 2000 ni moja ya migodi mikubwa zaidi ya dhahabu ya AngloGold Ashanti iliyo katika mabara matatu, huku uzalishaji mwaka huu ukitarajiwa kuwa takriban wakia 500,000.
AngloGold Ashanti imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza migodi ya chini ya ardhi kwenye mkataba wa GGML katika ukanda wa dhahabu wa Ziwa Victoria nchini Tanzania.
Maeneo matatu mapya ya uchimbaji chini kwa chini pamoja na uchimbaji mpya mmoja unaotumia mfumo wa wazi, ni moja ya maeneo yaliyochangia pakubwa uzalishaji wa dhahabu GGML katika kipindi cha miaka minne. Uwekezaji wa mtaji uliofanywa na GGML mnamo 2023 unatarajiwa kuwa ulifikia takriban Dola za Marekani milioni 193.
Miradi hii itaongeza maisha ya mgodi kwa miaka kadhaa. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, mpango wa utafiti wa kina kwenye maeneo mgodi ya GGML umepata mafanikio kwa kuongeza wakia milioni 4.8 iliyoongezwa kwenye hifadhi ya madini ikilinganishwa na wakia milioni 2.7 iliyozalishwa kwa wakati huo.
Mwaka 2023 Kampuni hiyo imewekeza Dola za Marekani milioni 35 katika utafiti katika eneo la mgodi pekee na imejitolea kuwekeza zaidi ya Dola za Marekani milioni 31 kwa mwaka 2024 kama sehemu ya kampeni yake ya kupanua zaidi maisha ya mgodi huu muhimu.
“Tumejitolea kuimarisha shughuli za GGML na wadau wake nchini Tanzania kuwa endelevu zaidi,” alisema Calderon na kuongeza; “Mgodi huu upo kwenye mpango wetu wa muda mrefu katika kampuni zetu zinazomilikiwa na AngloGold Ashanti na nia yetu ni kuiga mafanikio ambayo tumefurahia hapa na kuyasambaza katika migodi mingine na kuendeleza ugunduzi mwingine kama huo nchini Tanzania.”
Sambamba na mkakati endelevu wa AngloGold Ashanti wa kupunguza hewa ya ukaa, GGML inatekeleza mradi wa kuunganisha mgodi huo kwenye gridi ya Taifa ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), mpango ambao sio tu kwamba utapunguza nusu ya gharama ya uendeshaji mgodi lakini pia utakuwa na uwezo wa kupunguza utoaji wake wa kaboni kwa 81Kt CO2-e ifikapo 2030.
AngloGold Ashanti inaipongeza Serikali ya Tanzania kwa uwekezaji wake katika kuboresha gridi ya taifa kwani ni jambo ambalo litaongeza ufanisi katika upatikanaji wa nishati ya umeme na kupunguza gharama za matumizi ya umeme kwa kampuni nyingi.
Katika sehemu ya mchango wake katika kuleta thamani ya pamoja na jamii mwenyeji kwa ujumla, GGM tangu kuanzishwa kwake imeshirikiana na serikali kufadhili na kutekeleza miradi ya uwekezaji ya kijamii katika sekta za kimkakati kama vile elimu, afya, maji, barabara na mapato kwa kizazi kijacho.
Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu ambayo imekuwa kitovu cha ubora kwa wasichana katika ukanda wa Ziwa, sasa inachukua zaidi ya wasichana
1,000 kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
Mradi wa maji safi wa Mji wa Geita na Mradi wa Maji wa Mji huo kwa pamoja umesaidia kuinua idadi ya kaya zinazopata maji safi na salama kwa zaidi ya asilimia 65. Miradi hii, pamoja na dazeni ya mingine iliyofanywa kutokana na uwepo wa GGML, inaonyesha dhamira ya AngloGold Ashanti kuinua ustawi wa jamii ya Geita.
GGML imetambulika kwa mchango wake katika ustawi wa jamii, ikipokea tuzo mfululizo kutoka kwa Wizara ya Madini kuwa ndiyo iliyofanya vyema katika sekta ya madini kwa uwekezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii, utunzaji wa mazingira, ukuzaji wa biashara za ndani na usalama kazini.
Pia GGML pia ilipokea tuzo za Walaji (Consumer ChoiceAward) Tanzania kama kampuni inayoaminika zaidi kwenye sekta ya madini barani Afrika. “Tunapoendelea kuwekeza nchini Tanzania, GGML inajitahidi kuunda na kudumisha ushirikiano wa kudumu ili kusaidia maisha na biashara ambazo zitaishi zaidi ya muda wa mgodi huu,” alisema Calderon.