Featured Makala

MAJALIWA AMPONGEZA RAIS DKT.MWINYI KUYATEKELEZA MALENGO YA MAPINDUZI KWA VITENDO

Written by mzalendo

MAADHIMISHO ya kumbukumbu ya     Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964 ni muhimu sana kwani yanaukumbusha umma wa Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla kuhusu uzalendo uliofanywa na waasisi wa Taifa hili katika kuwatetea wananchi wanyonge.

Ni ukweli usiopingika kuwa historia inachangia kujaza moyo wa uzalendo kwa wananchi kwani huwafanya waone thamani ya kila hatua ya maendeleo Kwa maneno mengine historia ina mchango mkubwa katika kuongeza ari kwa wananchi kuitumikia nchi yao na kujiletea maendeleo pamoja na kuthamini kazi kubwa iliyofanywa na waliotangulia.

“Ninafahamu wengi wetu hasa makundi ya vijana hatukuwepo wakati Mapinduzi ya Mwaka 1964 yanafanyika licha ya kuwa ndio tumekuwa wafaidika wakubwa wa Mapinduzi yale.  Hivyo basi, sisi sote hatuna budi kuyaenzi Mapinduzi hayo matukufu na kuendelea kuyatetea na kuyalinda kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vile vijavyo.”

Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Jumatano, Januari 10, baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Skuli ya Muungano iliyopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar. Skuli hiyo ambayo itakuwa na madarasa 41 itagharimu shilingi bilioni 6.1 mpaka kukamilika kwake. Uwekaji huo wa jiwe la msingi ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Alisema maadhimisho hayo ni fursa kwa vijana kufahamu historia ya nchi yao. “Sote tunafahamu kuwa Mapinduzi yanafundishwa katika somo la historia, lakini kupitia mikusanyiko kama hii na mwendelezo wa mijadala inayofanyika katika kipindi kama hiki inaongeza ufahamu zaidi kwa jamii yote. Lakini pia ni ishara ya kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar na kuthamini jitihada iliyofanywa na wazee wetu katika kutuletea uhuru.”

Mheshimiwa Majaliwa alisema kupitia Mapinduzi ya Mwaka 1964, Zanzibar imeweza kupiga hatua kubwa katika kuwaletea wananchi wote maendeleo bila ya ubaguzi wa aina yoyote kwani kabla ya Mapinduzi hakukuwa na fursa sawa katika upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo huduma ya elimu.

Alisema awali shule zilikuwa chache na hivyo elimu ilikuwa ikitolewa kwa misingi ya kibaguzi kutegemea na matabaka na jamii kubwa ya Wazanzibar na watoto kutoka familia za kinyonge zilikosa fursa ya kupata elimu, kwa wale wachache waliobahatika basi walisoma katika shule zenye hadhi za chini kabisa. “Kwa msingi huo sina shaka mtakubaliana nami kuwa ilikuwa ni lazima mapinduzi yafanywe ili kuleta usawa kwa Wazanzibar wote.”

”…Kama mnavyofahamu, sababu kubwa ya kufanyika Mapinduzi ilikuwa ni kuchoshwa na hali ya ubaguzi mkubwa wa utawala wa kikoloni. Na huu ndio msukumo uliosababisha Mwezi Januari 1964, Wazanzibar walishikamana na kuamua kwa pamoja kuuondoa na kujiweka huru na udhalilishaji na madhila waliokuwa wakifanyiwa. Wazanzibar walipambana kumuondoa mkoloni kwa kufanya Mapinduzi ambayo leo hii tunajivunia kutimiza miaka 60 kwa kupiga hatua mbalimbali za Maendeleo.”

Aliongeza kwa kusema kuwa, “Uhuru tulionao sisi sote katika wakati huu umetokana na   ndugu zetu waliojitolea, wakiongozwa na Jemedari wa Mapinduzi Hayati Mzee Abeid Amani Karume, Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi. Hivyo basi, sote hatuna budi kuijua vizuri historia hii, kuiheshimu na kutoisahau katika maisha yetu kwa kurithisha vizazi na vizazi, kuilinda na kutorudi nyuma.” 

Mheshimiwa Majaliwa alisema maadhimisho hayo yanawakumbusha mwisho wa utawala wa kibeberu kwani Mapinduzi ya mwaka 1964 yalifanywa ili kuuondoa utawala wa kikoloni na kujitawala wenyewe wakiwa huru katika kujiletea maendeleo yao ya kijamii, kiuchumi na kisiasa hasa katika ulimwengu huu wa karne ya 21 ya sayansi na teknolojia.

Mapinduzi ya 1964 yamefungua fursa za huduma mbalimbali za maendeleo ya kijamii na kiuchumi Zanzibar zikiwemo elimu. Serikali huru ya Zanzibar katika kuendeleza misingi ya mapinduzi imeendelea kufanya mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma mbalimbali za jamii kwa wananchi wake ili wafaidi matunda ya uhuru wao.

MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA ELIMU

Waziri Mkuu alisema historia ya mageuzi katika sekta ya elimu ilianza tarehe 23 Septemba 1964, ambapo Serikali ya Mapinduzi iliyoongozwa na Hayati Mzee Abeid Aman Karume, Mwenyezi Mungu amrehemu, ilitangaza elimu bure kwa wananchi wote bila kujali rangi, kabila, dini, eneo wanalotoka au hata jinsia., mpango wa elimu bure umeendelea kudumishwa katika awamu zote za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi leo tunapoadhimisha miaka 60 sasa tangu kufanyika Mapinduzi hayo.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kueleza baadhi ya mafanikio yaliyopatikana upande wa sekta ya elimu katika kipindi cha miaka 60 ya Mapinduzi kuwa pamoja na uwepo  wa vyuo saba vinavyotoa masomo ya ngazi ya elimu ya juu ambapo kabla ya Mapinduzi hakukuwa na Chuo Kikuu hata kimoja.

Alisema vijana mbalimbali wanaomaliza masomo yao ya sekondari sasa wanapata fursa ya kujiunga na masomo ya vyuo vikuu ndani na nje ya Tanzania, ambapo katika kipindi hiki, idadi ya wanafunzi waliosajiliwa katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) pekee imefikia wanafunzi 7,250 mwaka huu wa 2023 kutoka wanafunzi 53 mwaka 2000 kilipoanzishwa.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali imefanikisha kuanzisha Tawi la Chuo cha Teknolojia, Institute of Technology Madrsa (IITM) cha India ambacho ndio chuo cha kwanza kwa ubora nchini India. “Uwepo wa chuo hiki kunaifanya Zanzibar kuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuwa na Tawi la chuo hicho na hivyo kutoa fursa kubwa kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla Kimataifa.”

Alisema uanzishwaji wa chuo hiko ni katika hatua ya utekelezaji wa Dira ya Maendelo ya Zanzibar ya 2050 inayoelekeza kuimarisha ujuzi na utaalamu kwa wananchi katika kufikia uchumi na jamii ilio bora na chuo hicho kitatoa wataalamu waliobobea kwenye masuala ya teknolojia na hivyo kuwa chachu ya utatuzi wa changamoto zinazolikabili Taifa katika sekta mbalimbali kama vile nishati, kilimo, afya, elimu na viwanda.

“Kama mlivyosikia hapo awali, fursa za upatikanaji wa elimu zilikuwa chache katika ngazi zote lakini kutokana na jitihada kubwa zinazondelea kufanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mageuzi makubwa yamefanyika katika kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa kuongeza miundombinu ya elimu, ambapo sasa Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyuo vitano vya kisasa vya mafunzo ya Amali kote nchini.”

Alisema ujenzi wa vyuo hivyo utakamilisha shabaha ya Serikali kuwa na Chuo cha Amali kikubwa na cha kisasa katika kila wilaya kwa lengo la kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na utaalamu utakaowasaidia kukabiliana na ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi hasa katika fani za Uchumi wa Buluu. Aidha, kupitia mradi huo, Serikali itajenga na kukipatia vifaa chuo cha ubaharia na kutanua Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ili kuongeza fani mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho zikiwemo mafuta na gesi.

“Pia, Serikali inajenga ofisi za elimu za wilaya na kuzipatia vifaa ambazo mbili tayari zimeshafunguliwa katika sherehe hizi zinazoendelea za maadhimisho ya kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi. Ujenzi wa ofisi hizi utaimarisha ufuatiliaji na usimamizi katika utoaji na upatikanaji wa elimu bora. Kuziunganisha Skuli zote na mkonga wa taifa wa mawasiliano ili kuimarisha matumizi ya teknolojia katika kufundishia na kujifunzia.”

MAFANIKIO KATIKA SEKTA YA AFYA

 

Waziri Mkuu alisema Mheshimiwa Rais Dkt Mwinyi amedhamiria kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma katika mazingira bora na kwa viwango vinavyokubalika ikiwa ni pamoja na kuendelea kuweka mifumo imara ikiwemo mfumo wa rufaa utakaozingatia huduma bora zinazotolewa kwa wakati.

Alisema miradi ya ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya inatekelezwa ili kusogeza huduma bora karibu na wananchi,  kupunguza msongamano na kufanya utoaji wa huduma za afya uwe rafiki kwa watoa huduma na kwa wananchi na kwamba ujenzi wa vituo vya kisasa vya kutolea huduma za afya utapunguza gharama kutokana na ukweli kwamba, kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kugharamia matibabu ya wananchi nje ya nchi.

“Serikali imeanza na itaendelea kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya ili madaktari bingwa na bobezi wazalendo na wale wa kigeni waweze kuwa na mazingira rafiki ya kutoa huduma za kibingwa na kibobezi katika hospitali zetu za kisasa zilizopo hapa nchini.”

 

Waziri Mkuu alisema kutokana na jitihada hizo, Serikali imeshajenga hospitali 10 za wilaya katika wilaya za Unguja na Pemba, na kila hospitali ina vifaa tiba kamili na magari ya kisasa ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya kutoa tiba stahiki za dharura na rufaa.  Hospitali hizo zote ni nzuri na zina huduma zote za kisasa kama lilivyo jengo hili la Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini B. Aliyasema hayo wakati akifungua Hospitali ya wilaya ya Kaskazini B Pangatupu iliyopo mkoa wa Kaskazini Unguja.

“Mradi huu wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini B ni matokeo ya mipango thabiti na utekelezaji wa ahadi ya Serikali yetu Tukufu zinazokwenda sambamba na utekelezaji wa mikakati ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964. Serikali iliahidi itatekeleza na leo tumefungua hospitali hii mpya ambayo ina hadhi ya wilaya na itatoa huduma za afya kwa mfumo wa kidijitali.”

PONGEZI KWA RAIS DKT. MWINYI

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuyaendeleza na kutekeleza malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi ni kiongozi mwenye busara, hekima na mchapakazi mwenye kuwatumikia wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo wanayoyataka kwa kasi kubwa. Kila mmoja wenu ni shahidi wa mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yaliyofanyika Zanzibar katika kipindi kifupi.

Mbali ya hayo Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi ameendeleza umoja, mshikamano, amani na utulivu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ambayo imekuwa kichocheo katika kutekeleza shughuli mbalimbali za kuwaletea wananchi Maendeleo. Mwenyezi Mungu amzidishie afya njema hekima na busara katika kuwatumikia zaidi wananchi. Haya ndio malengo hasa ya mapinduzi.”

Naye, Waziri wa Afya, Nassoro Ahmed Mazrui alisema takwimu zinaonesha Zanzibar kuna mapinduzi makubwa ya huduma za afya katika sekta ya umma kwani wametoka kuwa na vitanda 1,445 vya kulaza wagonjwa na sasa vipo takribani vitanda 2,645 vya kulaza wagonjwa katika hospitali za Unguja na Pemba.

Alisema awali kulikuwa na ICU moja tu ya Hospitali ya Mnazimmoja, yenye vitanda vinane na sasa hivi kuna jumla ya ICU 14 na vitanda 80 vya ICU ikiwa ni pamoja na vitanda sita vya ICU vilivyokuwemo ndani hospitali ya wilaya ya Magharibi A. Pia kulikuwa na vyumba vya upasuaji 11 na kati yake  viwili ni maalum kwa ajili ya akina mama wenye mahitaji ya kujifungua kwa upasuaji na sasa hivi kuna vyumba 35 vya upasuaji vikiwemo 13 maalum kwa ajili ya akina mama na vitengo vya dharura vimeongezeka  kutoka viwili hadi 13.

Awali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa alitumia fursa hiyo kutaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana upande wa sekta ya elimu katika kipindi cha miaka 60 ya Mapinduzi kuwa ni pamoja kuongezeka kwa Bajeti ya sekta ya elimu kutoka shilingi bilioni 265.5 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 457.2 katika mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 72.2.

Alisema kiwango hicho cha bajeti katika historia ya Zanzibar ni kielelezo cha dhamira ya Serikali katika kuendeleza Sekta ya Elimu, ambapo kwa sasa imejipanga kujenga shule 25 za ghorofa katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024; ikiwemo shule hiyo ya ghorofa tatu (G+3) ya Muungano.

Alisema mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule zinazotoa elimu ya maandalizi kutoka shule moja tu mwaka 1964 hadi kufikia skuli 891 mwaka 2023. Aidha katika kipindi hicho shule zinazotoa elimu ya msingi zimeongezeka kutoka 62 hadi 649, shule za Sekondari zimeongezeka kutoka tano na kufikia shule 318 mwaka 2023.  

“Uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi zote za elimu (Maandalizi, Msingi na Sekondari) umeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka wanafunzi 25,432 mwaka 1964 na kufikia wanafunzi 592,781 mwaka 2023. Ukuaji huu wa uandikishaji wa wanafunzi umetokana si tu kwa sababu ya ongezeko la idadi ya watu bali pia elimu kuwa ni haki ya msingi kwa kila mtoto.

Matokeo ya mitihani ya taifa kwa wanafunzi wetu yameimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu. Kwa Mwaka 2023, matokeo ya mitihani ya kidato cha nne asilimia ya ufaulu imeongezeka kutoka 55.4 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 74.0 mwaka 2022.”

Aidha, kwa upande wa ya Kidato cha Sita, matokeo ya mitihani yanaonesha kuwa, kati ya wanafunzi 2,587 waliofanya mtihani huo wanafunzi 2,570 sawa na asilimia 99.3 wamefaulu kuendelea na masomo ya chuo kikuu katika kiwango cha Divisheni I hadi 3. Kati yao, asilimia 65.9 wamefaulu katika masomo ya sayansi.

Pia, Waziri Lela alisema Serikali imefanya mapitio ya mitaala ya elimu ya maandalizi na msingi kukidhi mahitaji ya sasa ya kusoma kwa kuzingatia umahiri Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya mapitio pia kwa mtaala wa elimu ya Sekondari kukidhi mahitaji ya umahiri na kuimarisha elimu ya amali na ufundi.

About the author

mzalendo