Featured Kitaifa

ZAIDI YA ASILIMIA 74 YA WATANZANIA WANAPATA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA MSINGI

Written by mzalendo

Na. WAF – Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuboresha huduma za Afya ambapo kwa Mwaka 2023 zaidi ya asilimia 74 ya Watanzania wamepata huduma za Afya katika ngazi ya msingi (Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya pamoja na Halmashauri).

Waziri Ummy amesema hayo Januari 10, 2024 wakati akitoa taarifa ya hali ya utoaji huduma za Afya nchini kwa mwaka 2023 katika mkutano wake na Waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es salaam.

“Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kuongeza nguvu ya kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa utoaji wa huduma za Afya ngazi ya msingi ili Watanzania wengi wapate huduma bora zilizopo karibu nao.” Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kwa Mwaka 2023 mahudhurio ya wagonjwa wa nje (OPD) imeongezeka na kufikia Mil. 42,252,741 kutoka wagonjwa 41,347,690 kwa mwaka 2022.

“Katika mwaka 2023, Wagonjwa hawa wamepata huduma katika ngazi za Zahanati kwa 33%, Kituo cha Afya – 18%, Hospitali za Halmashauri – 23%, Hospitali za Rufaa za Mikoa – 9%, Hospitali za Rufaa za Kanda, Maalum na Taifa – 17%.” Amesema Waziri Ummy

Ameongeza kuwa Wagonjwa waliopata huduma ya Kulazwa (IPD) kwa Mwaka 2022 ni wagonjwa Mil. 1,630,722 na Mwaka 2023 kulikuwa na wagonjwa Mil. 1,622,979.

“Mwaka 2023, wagonjwa hawa wamepata huduma katika ngazi za Kituo cha Afya – 26%, Hospitali za Halmashauri – 51%, Hospitali za Rufaa za Mikoa – 13%, Hospitali za Rufaa za Kanda, Maalum na Taifa – 10%.” Amesema Waziri Ummy

About the author

mzalendo