Featured Kitaifa

MWAKA 2023 WAGONJWA 15,386 WAMEPATA HUDUMA MPYA ZA CT-SCAN HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA

Written by mzalendoeditor

Na. WAF – Dar es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema katika mwaka 2023 wagonjwa 15,386 walipata huduma za CT – Scan katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ambapo hapo awali huduma hiyo ilikuwa haipatikani katika Hospitali hizo.

Waziri Ummy amesema hayo Januari 10, 2024 wakati akitoa taarifa ya hali ya utoaji huduma za Afya nchini kwa mwaka 2023 katika mkutano wake na Waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es salaam.

“Uwekezaji huu umeleta mabadiliko makubwa katika huduma za uchunguzi wa magonjwa na hivyo kupelekea huduma hizi kuwafikia wananchi kwa urahisi katika maeneo wanayoishi na kupunguza usumbufu wa kupoteza muda na gharama za kupata matibabu.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy wakati akiendelea kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Afya Mwaka 2023 amesema mashine ya kuchunguza magonjwa kama ya misuli, mishipa ya damu na fahamu, ubongo na vivimbe (MRI) zimeongezeka kufikia 13 ambapo awali (Mwaka 2022) zilikua Sita.

“Lakini pia, mashine ya kuchunguza magonjwa ya misuli, ubongo, viungo vya mwili (CT SCAN ) zimeongezeka kufikia 45 Mwaka 2023 ambapo awali zilikua 22 tu.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, pamoja na mashine za Digital X- Ray zimeongezeka kufikia 346 na zote zinafanya kazi ambapo kwa Mwaka 2022 zilikua mashine 296 pamoja na mashine za Utra Sound, Disemba 2022 zilikuwa 192 huku Disemba 2023 zimefikia 512 ongezeko la mashine 320.

About the author

mzalendoeditor