Uwepo wodi ya watoto wanaohitaji uangalizi maalum (PICU) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili umesaidia kuokoa maisha ya watoto ambao walikuwa wanapoteza maisha hapo awali kutokana na ukosefu wa huduma hiyo.
Daktari Bingwa wa Watoto, Dkt. Namala Mkopi ambaye pia ni Mkuu wa Wodi hiyo amesema huduma katika eneo hilo hutolewa kwa watoto wote ambao wako katika hali mahututi na wale ambao wametoka kufanyiwa upasuaji mkubwa na wanahitaji kuangaliwa kwa ukaribu zaidi.
Dkt. Mkopi ameongeza kuwa kuanzishwa kwa wodi ya PICU kumewezesha kufanyika kwa huduma za upasuaji za kibingwa na bobezi ambazo awali zilikuwa hazifanyiki kutokana na ukosefu wa wodi ya uangalizi maalumu na wakati mwingine zilikuwa zinafanyika kwa mashaka kwa sababu huduma za uangalizi wa karibu kwa watoto ulikuwa wa mashaka.
“Tangu tumeanzisha wodi hii mwaka 2019 tumeweza kuokoa maisha ya watoto ambao awali walikuwa wanafariki kwa kukosa huduma za uangalizi wa maalum kwani ilitulazimu kuwalaza watoto hao katika PICU ya watu wazima ila tangu tumeanzisha kitengo hiki tumeokoa maisha ya watoto wengi,” amefafanua Dkt. Mkopi.
Pamoja na hayo ameongeza kuwa PICU ina jukumu la kutoa elimu kwa wataalam wengine wanaohudumiwa watoto katika maeneo mengine hospitalini hapo kuhakikisha kuwa wanagundua mapema watoto ambao wanahitaji kupatiwa uangalizi wa karibu na kuwapelekeka katika kitengo hicho kwa wakati ili wapatiwe huduma stahiki na kuokoa maisha yao.
Kwa upande mwingine ameeleza kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ndio hospitali ya kwanza kuanzisha huduma hiyo nchini hivyo imekuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa inawajengea uwezo wataalamu wa hospitali nyingine sehemu mbalimbali nchini ili kutoa huduma kama hizo katika maeneo yao na kusaidia kuokoa maisha ya watoto hao.
“Tuna jukumu kubwa kama hospitali ya taifa kuhakikisha kwamba sio tu Muhimbili inaokoa maisha ya watoto mahututi bali hata sehemu nyingine ambazo wanatoa huduma kwa watoto hivyo katika kufanikisha hili tunatoa elimu kwa hospitali zingine ambazo zinataka kuanzisha kitengo kama hiki,” amesema Dkt. Mkopi.
Dkt. Mkopi ametaja kuwa watoto wengi wanaolazwa PICU ni pamoja na wenye magonjwa ya kuambukiza, waliofanyiwa upasuaji mkubwa, wenye saratani na magonjwa mengine ambao hupata huduma kutoka kwa watalaam mseto wakiwemo madaktari bingwa wa watoto, madaktari bingwa wa watoto mahututi, madaktari wa kawaida, wataalamu wa utengamao, wataalamu wa lishe pamoja na wauguzi waliobobea.