Na. Majid Abdulkarim, Dodoma
Waganga wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini wametakiwa kuhakikisha wanabainisha vipaumbele vya Taasisi zao kulingana na vipaumbele vya sekta ya afya kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuleta ubora wa Huduma za afya nchini.

Rai hiyo imetolewa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa huduma za tiba Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo katika kikao cha Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kupitia Mapendekezo ya Mpango wa Bajeti kwa Mwaka 2024/2025.

Prof. Ruggajo amesema kuwa katika mpango wa bajeti ya mwaka 2024/25 za Hospitali zote nchini lazima ziendane na vipaumbele vya sekta ya afya ili wanachi waweze kunufaika na Huduma zinazotolewa Hospitalini.

“Lakini hakikisheni mnafanya utafiti na kutoa matokeo ya utafiti mnaofanya ili kuleta tija ya tafiti hizo kwa jamii na taifa kwa ujumla kwani tafiti pia ni sehemu ya utendaji wenu”. Amesisitiza Prof. Ruggajo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti Wizara ya Afya Bw. Lusajo Ndagile amesema kuwa lengo la kikao hicho ni maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2024/25 pamoja na kuwajengea uwezo waganga wafawidhi hao kuandaa Mpango na Bajeti.

Pia Bw. Lusajo amesema kuwa wametumia kikao hicho kuwapitisha waganga wafawidhi hao katika mpango mkakati wa Wizara ya Afya

“Vile vile wamepata mafunzo ya muongozo juu ya Mpango na bajeti ili kuleta ufanisi wakati wa kuaanda bajeti za taasisi zao”. ameeleza Bw.Lusajo.

Aidha, Bw. Lusajo huyo amesema kikao hicho ni mwendelezo baada ya kikao cha jana kilichowakutanisha Wakurugenzi wa Fedha na Mipango kutoka Taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Afya.

Previous articleMAJIMBO 214 KUNUFAIKA NA UGAWAJI WA VIFAA TIBA VYA SHILINGI BILIONI 14.9
Next articleWAZIRI MAVUNDE AAINISHA MAMBO MUHIMU KUFIKIA MALENGO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here