Featured Kitaifa

SHUWASA YAJIVUNIA MAFANIKIO MAKUBWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAJI

Written by mzalendo
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya SHUWASA kwenye mkutano na waandishi wa habari leo Alhamisi Januari 4,2024. Kushoto ni Afisa Mahusiano kwa Umma SHUWASA bi. Nsianel Gelard
Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano ulioandaliwa na SHUWASA kwa ajili ya taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya SHUWASA
Na Eunice Kanumba na Kadama Malunde – Shinyanga
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) imeeleza mafanikio makubwa iliyoyafikia ndani ya kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi mwaka 2022/2023 (Miaka mitatu ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan) ambayo ni pamoja na kupanua mtandao wa maji safi, kuongeza mapato yatokanayo na mauzo ya maji, kuongeza idadi ya wateja, kupunguza upotevu wa maji na ujenzi na utekelezaji wa miradi kabambe ya maji.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Januari 4,2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya SHUWASA kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi mwaka 2022/2023 jumla ya shilingi 8,595,802,786 zilitumika katika ujenzi wa miradi na wanufaika wapatao 116,249 wanafaidika na miradi hii ambapo jumla ya miradi 10 imetekelezwa, miradi 7 imekamilika na miradi mitatu inaendelea kutekelezwa na inatarajiwa kukamilika ifikapo Mwezi Februari 2024.
Aidha amesema hali ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa sasa ni nzuri katika maeneo yote wanayoyahudumia kutokana na kwamba hivi sasa wanapata maji ya uhakika kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama na Shinyanga (KASHWASA).
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya SHUWASA.
Amesema SHUWASA ambayo inajihusisha na utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa Mazingira katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na Miji midogo ya Tinde, Didia na Iselamagazi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga , kuanzia mwaka 2020/2021 hadi mwaka 2022/2023 idadi ya wateja imeongezeka kutoka 24,580 mwezi Juni 2021 hadi kufikia 28,672 sawa na ongezeko la wateja 4,092 mwezi Juni 2023.
“Kwa sasa SHUWASA ina jumla ya wateja 30,135 na tunatarajia kuongeza wateja na kufikia 32,000 mwezi Juni 2024.
Tumeboresha mahusiano kwa wadau mbalimbali wa ndani na wa wadau wa nje”,ameeleza Mhandisi Katopola.
Kuhusu potevu wa Maji, SHUWASA
imefanikiwa kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 26 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi asilimia 20% kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
 
“Mwaka 2021/2022 tulifanikiwa kupata tuzo ya Mamlaka bora katika Mamlaka 26 za Mikoa katika Udhibiti wa upotevu wa maji kwa kuwa na upotevu wa asilimia 16%. Kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 hadi mwezi Desemba 2023, Mamlaka iko na upotevu wa maji asilimia 11%”,amefafanua Mhandisi Katopola.
 
WIZI WA MAJI
Mkurugenzi huyo wa SHUWASA amesema wamefanikiwa kukamata wezi wa maji wapatao 76 kati ya mwaka wa fedha 2021/2022 na mwaka wa fedha 2022/2023 na kuwakadiria adhabu inayofikia Tzs 29,161,858.
MAUZO YA MAJI
Katika Mwaka wa fedha 2020/2021, amesema mauzo ya maji yalikuwa shilingi 6,337,659,070.00, Mwaka wa fedha 2022/2023 mauzo ya maji yalikuwa 8, shilingi 789,159,353.00 sawa na ongezeko la shilingi 2, 451,500,283 ikiwa ni ongezeko la asilimia 27.89%.
“Kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 hadi Desemba 2023 mauzo ya maji yalikuwa 5, 233,547,797. Matarajio yetu ya kuuza maji (Billing) yanayofikia kiasi cha shilingi 10,730,296,792”,ameongeza Mhandisi Katopola.
 
MAPATO YATOKANAYO NA MAUZO YA MAJI
Mhandisi Katopola amesema katika mwaka wa fedha 2020/2021 mapato yalikuwa Shilingi 6,713,002,426, na mwaka wa fedha 2022/2023 mapato yalikuwa shilingi 8,165,297,101 na kwamba SHUWASA inazidai taasisi mbalimbali kiasi cha shilingi 906,428,713.00 huku akibainisha kuwa ongezeko la mapato ni shilingi 1,452,294,674 sawa na asilimia 17.78%.
UTEKELEZAJI MIRADI MIKUBWA
Mhandisi Katopola miradi mikubwa inatarajiwa kutekelezwa ikiwemo mradi wa IFF – OBA na mradi wa AFD ambapo jumla ya shilingi milioni 735, 464,939 zitatumika katika ujenzi wa mradi wa (IFF – OBA) wa kuchakata majitaka kufikia mita za ujazo 100 kwa siku.
Ameeleza kuwa kwa sasa SHUWASA ina uwezo wa kutibu majitaka kwa mita za ujazo 40 na mamlaka hiyo ipo katika hatua ya ununuzi wa gari la majitaka kama sehemu ya usimamizi wa mazingira.
Kuhusu Mradi wa AFD, amesema Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha ilisaini Mkataba wa fedha na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (French Development Agency – AFD) kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa eneo linalohudumiwa na SHUWASA na kwamba mkataba huu wenye thamani ya EURO milioni 76 (Euro 75 ni mkopo wa riba nafuu toka Shirika la Maendeleo la Ufaransa na Euro milioni 1 zitatolewa na Serikali ya Tanzania) ulisainiwa mnamo tarehe 20.06.2022. Mkataba huu wa fedha unatarajiwa kuanza rasmi mwezi Mei 2024 kufikia tamati mwezi Mei mwaka 2028.
“SHUWASA inaendelea na utekelezaji wa mradi huu ambao unahusisha, ujenzi wa Mtandao wa majisafi kwa kilomita 298,
 ukarabati wa mtandao chakavu wa majisafi kwa takribani kilomita 100 na ujenzi wa matangi mawili ya kuhifadhia majisafi yenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 1,500 eneo la Kolandoto na mita za ujazo 250 eneo la Didia”, ameeleza Mhandisi Katopola.
Kazi zingine zinazoendelea ni ujenzi wa mitambo minne ya kuchakata tope kinyesi eneo la Ihapa na Mwagala kwa Manispaa ya Shinyanga na Kituli na Iselamagazi – Halmashauri Wilaya ya Shinyanga, ukarabati wa Mtambo wa kutibu maji Ning’hwa na tathmini ya Ufanisi na ukarabati wa bwawa la Ning’hwa na kuijengea uwezo SHUWASA ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo jipya la ofisi.
Mhandisi Katopola amesema tayari SHUWASA imeshatangaza zabuni mbili za kupata wahandisi washauri kwa eneo la Ujenzi na Usimamizi (Design & Supervision) pamoja na eneo la Usaidizi kwa Mamlaka (Technical Assistance) kwa usimamizi wa Mradi na zabuni moja ya kandarasi ya ujenzi (Construction of portable water infrastructure) ambazo ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Pia SHUWASA inaendelea na zoezi la kurasimisha maeneo mbalimbali ya mradi, ambapo maombi ya fedha za fidia kwa waathirika wa mradi yamewasilishwa Wizara ya Maji mnamo tarehe 24.10.2023 kwa hatua zaidi za utekelezaji.
Ameongeza kuwa kwa sasa SHUWASA inaendelea na maandalizi ya nyaraka mbalimbali za mradi ikiwa ni pamoja na maombi ya vibali mbalimbali kutoka kwa mfadhili na Taasisi nyingine za Serikali ili kuwezesha mikataba ya shughuli za ujenzi kusainiwa na utekelezaji kuanza.
 
“Imetazamiwa kuwa mkandarasi atakabidhiwa eneo la mradi na kuanza shughuli za ujenzi mwezi Machi, 2024. Mradi utahusiha ujenzi wa vyoo vya kisasa katika maeneo ya kijamii kama shule, vituo vya afya, stendi vipatavyo 36. Kuijengea uwezo SHUWASA ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la Ofisi”,ameongeza.

About the author

mzalendo