Kitaifa

TNMC YAWATAKA WAUGUZI NA WAKUNGA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA KIAPO CHAO

Written by mzalendo

Na. Gideon Gregory, Dodoma.

Baraza la Uuguzi na Ukunga nchini (TNMC)limetoa rai kwa wauguzi na wakunga nchini kufanya kazi zao kwakukuzingatia kiapo cha maadili ya kazi zao katika kusimamia miiko ya taaluma zao ili kutoa huduma bora kwa jamii. 

Kaimu Msajili wa Baraza hilo, Happy Masenga ametoa rai hiyo leo Desemba 27,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu kufanyika kwa Mtihani wa usajili na leseni kwa wauguzi na wakunga Tanzania Bara.

“Naomba nitoe wito kwa wauguzi na wakunga waliopo kazini kuzingatia maadili na kiapo cha taaluma ya uuguzi na ukunga ili kuepukana na matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara,”amesema.

Aidha Bi. Masenga amewataka watahiniwa wote waliojisajili kwa ajili ya mtihani huo kufika katika vituo walivyoomba siku ya kesho Desemba,28 ili kupata maelekezo na namba zao za mtihani.

“Mtihani huu unatarajiwa kufanyika Desemba 29 katika vituo mbalimbali vilivyo tambuliwa na kukubalika na Baraza katika mikoa Saba hapa nchini”,amesema.

Jumla ya watahiniwa 4166 wamekidhi sifa za kufanya mtihani huo wakiwemo 3917 ambao wanafanya mtihani kwa mara ya kwanza,na 248 wanaorudia.

About the author

mzalendo