Kitaifa

SHERIA YA MAJENGO NCHINI KUWEZESHA KUWEPO KWA MFUMO WA PAMOJA WA USIMAMIZI WA UJENZI WA MAJENGO – MHA. MWAKASEGA

Written by mzalendo

Na. Gideon Gregory, Dodoma.

Mhandisi Ujenzi katika baraza la taifa la Ujenzi (NCC) Geofrey Mwakasenga amesema kuwa uwepo wa sheria ya majengo nchini utawezesha kuwepo kwa mfumo wa pamoja wa usimamizi wa ujenzi wa majengo wenye uwezo wa kudhibiti uharibifu wa mazingira, ubora, usalama na afya.

Mhandisi Mwakasenga ameyasema hayo leo Desemba 21,2023 Jijini Dodoma wakati akizungumza na na waandishi wa habari wakati akielezea masuala muhimu kuhusu sheria ya majengo nchini ambapo NCC inaratibu uandaaji wake.

“Kwasasa ujenzi wa majengo unasimamiwa na sheria nyingi mbalimbali kwasababu ya kukosekana sheria moja maalum, hivyo kusababisha usumbufu katika uendelezaji wa majengo na gharama zisizo za lazima kwa wandelezaji wa majengo,”amesema.

Amesema baadhi ya sheria zinazosimamia ujenzi wa majengo nchini ni pamoja na sheria za mipango miji, afya na usalama mahali pa kazi, zimamoto na uokoaji, mazingira, ukandarasi na usajili pamoja sheria zinazosimamia taaluma na wanataaluma katika fani ya za uhandisi, ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi.

“Sheria hizi zinatoa mwongozo katika baadhi ya maeneno na kuyaacha mengine bila usimamizi, jambo linaloifanya sekta ndogo ya ujenzi wa majengo inayohusiana pia na ubomoaji wa majengo kutosimamiwa ipasavyo,”amesema.

Ameongeza kuwa kulingana na jukumu ambalo baraza hilo imepewa la kuratibu uandaaji wa sheria ya majengo nchini NCC imekamilisha mchakato wa kuandaa andiko dhana linaloainisha umuhimu wa sekta ya ujenzi pamoja na changamoto zinazojitokeza kwa sasa.

Sambamba na hayo amesema majukumu mengine ambayo NCC inafanya ni kuhamasisha ubora katika sekta ya ujenzi ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa kiufundi wa miradi ya ujenzi.

“Pia NCC inahamasisha mbinu za ujenzi zenye kuzingatia uhifadhi endelevu wa mazingira pamoja na afya na usalama wa kazi katika shughuli za ujenzi,”amesema.

Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha mawasiliano NCC Eliezer Rweikiza amesema kuwa sheria ya majengo imeboreshwa ili vitu ambavyo havikuwa kwenye sheria zilizopita ziweze kuingizwa ndani.

“Zipo taasisi zinazosimamia wakandarasi, wahandisi na watu wanaohusika katika sekta ya ujenzi, na sheria inapokuja inamaana kuwa mapungufu yaliyoko kule yanawekwa pamoja ili yaweze kufanyiwa kazi na hilo jukumu litwakuwa linasimamiwa na kuratibiwa na NCC,”amesema.

About the author

mzalendo