Na Mwandishi wetu – Dodoma.
Watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuathiri utendaji wa majukumu ya Tume hiyo kama rushwa, ulevi, na uvunjifu wa maadili katika Utumishi wa Umma.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya NEC uliopo Njedengwa Jijini Dodoma amewasihi kufuata maadili ya utumishi wa umma na kuzingatia kanuni na miongozo wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao.
Amewataka kuendeleza ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao hasa ikizingatiwa Tume hiyo ni taasisi nyeti na muhimu kwa Taifa hivyo hawana budi kudumisha mshikamano na ushirikiano kuwa nguzo yao muhimu ili kufanikisha majukumu yao kwa pamoja na kwa kasi zaidi.
“Fuateni maadili ya utumishi wa umma na kuishi viapo vyenu vya utunzaji siri, hasa ikizingatiwa mko katika taasisi nyeti na muhimu kwa Taifa letu. Mkashikamane na ushirikiano uwe ndiyo nguzo yetu, hii itasaidia kufanikisha majukumu yetu kwa pamoja na kwa kasi zaidi,”Amesema Mhe. Ummy.
Pia amewasisitiza kuzingatia katiba, sheria, kanuni na taratibu wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao kwa kuepuka matumizi ya lugha zozote za uchochezi zinazoweza kuleta uvunjifu wa amani.
Aidha amewaasa watumishi hao kuepuka kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa watumishi walioko katika Idara au Vitengo na wadau mbalimbali wa uchaguzi bali wajikite kufikisha taarifa zilizo sahihi na zinazokusudiwa kwa Watumishi na Wananchi wote kwa ujumla kwa kufuata utaratibu wa utoaji habari, na pia kuwahamasisha watumishi kujituma zaidi kuendana na kasi ya uongozi tuliyonayo kwa Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Tunashukuru sana kwa kujitoa kwenu na kuweza kukamilisha zoezi la uboreshaji wa majaribio lililofanyika kwa siku saba (7) katika Kata ya Ng’ambo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023, hakika mmetekeleza zoezi hili kwa nguvu na tumeonesha kwamba tumejipanga, tunaweza na tuko tayari na zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linalotarajia kuanza mapema mwaka 2024,”Amepongeza Mhe. Ummy.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima amelijulisha Baraza hilo kwamba uboreshaji wa majaribio umefanyika kwa mafanikio.
“Uboreshaji huo wa majaribio, Tume ilifanikiwa kupima uwezo wa vifaa na teknolojia ya uboreshaji ambalo ndilo lilikuwa lengo kuu la zoezi hilo na nitumie fursa hiii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuisimamia vyema tume hii,”