Kitaifa

ANGALIENI FURSA ZA UZALISHAJI KATIKA MAENEO YENU – DKT. MUSSA

Written by mzalendo

Na. Asila Twaha, Morogoro

Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji na Wiwanda, Biashara na Uwekezaji kuangalia fursa za uzalishaji zilizopo katika maeneo yao na kuzifanyia kazi kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi na wananchi.

Dkt. Mussa ameyasema hayo leo Mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji na Viwanda, Biashara na Uwekezaji yenye lengo la kuwakumbusha majukumu yao na kuwataka kuwa wabunifu na kujua fursa zilizopo katika maeneo walipo.

Amewataka wataalamu hao kufanya tafiti na kuzijua fursa za uzalishaji ambapo amesisitiza kuwa fursa hizo zilizopo ziandane na utoaji wa elimu kwa wananchi ili waweze kuzijua fursa zilizopo katika maeneo yao na kuzifanyia kazi kwa kushughulika nazo ili waone umuhimu na namna gani wataweza kuzitumia na kuwasaidia kujikwamua kimaisha na kukuza uchumi wao lakini pia kuongeza ukuaji wa uchumi wa nchi.

Dkt. Mussa amesema asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania shughuli zao ni kilimo hivyo wao kama wataalamu wanatakiwa kujua na kuona ni jinsi gani wataweza kuisaidia Serikali kwa kuwa wabunifu na kujua uzalishaji gani ulipo kwa ajili ya kuwa fursa za biashara na uwekezaji.

“tusiwe na mazoea ya kufanana kimazao kila eneo kuna neema yake ni vizuri mfikirie kitaalamu ili kuleta utofauti wa uzalishaji kwa ajili ya kuongeza uthamani wa eneo husika” alisema Dkt. Mussa.

Akieleza fursa zilizopo Mkoani Morogoro amesema, mbali ya kulima mazao mengine lakini pia wameweza kuangalia soko la viungo ambalo ni zao zuri la uwekezaji na wanaweza kuongeza kipato sio tu kwa wananchi bali na nchi kama zao la karafuu ambalo limezoeleka kulimwa Zanzibar lakini kwa Morogoro wamefanya tafiti na kuona zao hilo linaweza kulimwa na litaweza kuwasaidia wananchi wake.

Awali akieleza malengo ya mafunzo hayo Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Uratibu wa Shughuli za Serikali Bw. Johnson Nyingi amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI inaendelea kutoa mafunzo kwa maofisa wanaowasimamia kwa kuamini mafunzo wanayoyapata wataenda kufanya mabadiliko katika maeneo yao na kuwasaidia wananchi kukuza uchumi wao na maendeleo kwa ujumla.

About the author

mzalendo