Waziri MKuu, Kassim Majliwa akizungumza alipofunga Maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii kwenye Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Desemba 18, 2023.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amevitaka vyuo vinavyotoa elimu kuhusu masuala ya Ustawi wa Jamii nchini vifanye mapitio ya mitaala ili iendane na wakati na itoe majibu kwa changamoto za sasa za jamii sambamba na kufanya tafiti mbalimbali ikiwemo tafiti za masuala ya malezi na maadili.
Amesema Serikali ya awamu ya sita kwa upande wake itaendelea kutekeleza azma yake ya kuimarisha ustawi wa wananchi kwa kuendelea kufanya maboresho ya mifumo, ufuatiliaji na usimamizi wa masuala ya ustawi wa jamii sambamba na kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Desemba 18, 2023) kwenye kilele cha Wiki ya Ustawi wa Jamii na Maadhimisho ya Miaka 50 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii, ukumbi wa JNICC – Dar es Salaam. Amesema ipo haja ya kufanya tathmini ya mfumo mzima wa malezi na makuzi ya watoto na vijana ambayo ndio msingi mkuu wa kukuza maadili katika jamii.
”Wazazi, walezi na Watanzania kwa ujumla kila mmoja ashiriki katika kulinda haki na ustawi wa watoto wetu. Hii ni nguvukazi ya Taifa letu hivyo basi, ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu letu sote. Pia Wizara ikamilishe programu ya ulinzi wa kijamii (social protection application) ili ianze kutumika.”
Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya maadhimisho inayosema ’Malezi na Makuzi kwa Watoto na Vijana kwa Maendeleo ya Taifa’ ambayo itaambatana na mjadala wa kitaifa unaoakisi mada hiyo, Waziri Mkuu amesema mada hiyo ni thabiti na imekuja katika wakati muafaka.
”Nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine duniani inapitia changamoto ya ongezeko la vitendo vya mmomonyoko wa maadili unaochangiwa na mitindo ya maisha. Hakuna shaka kuwa mjadala huu utawezesha kupata uelewa wa pamoja kama Taifa ili kuweka mikakati ya kitaifa ya kukabiliana na changamoto ya mmomonyoko wa maadili.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kutokana na changamoto za kiuchumi familia nyingi zinashindwa kupata muda wa kutosha kulea watoto na vijana ambao ni muhimu katika ujenzi wa Taifa la sasa na baadaye, hivyo mada hiyo ni kengele ya amshaamsha kwa kila mtendaji na mwanajamii kutambua kuwa suala la malezi na makuzi ya watoto na vijana ni msingi wa maendeleo ya Taifa letu.
Vilevile, Waziri Mkuu amesema Maafisa Ustawi wa Jamii ni wasuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia, hivyo amewataka waongeze kasi ya kutoa huduma. ”Hivi karibuni kumekuwa na changamoto kubwa ya kuvunjika ndoa na kusababishwa ombwe katika malezi ya watoto. Tusaidieni kuimarisha taasisi ya familia ili watoto wapate malezi bora ya wazazi wote wawili.”
Waziri Mkuu amesema pasipo misingi bora ya malezi ya watoto na vijana Taifa halitaweza kupata ustawi bora wa jamii kama inavyotarajiwa, ambapo ametumia fursa hiyo kukumbusha wajibu wa taasisi zote zinazohusika na malezi ambazo ni familia, shule, madhehebu ya dini na jamii kwa ujumla kuweka kipaumbele katika suala la malezi na makuzi ya watoto na vijana ili waweze kujenga jamii wanayoitaka katika misingi ya uchumi, imani na uhusiano.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM mwaka 2020 – 2025 chini ya Ibara za 89 hadi 92 imebainisha kuwa kuinua na kuimarisha maisha ya mtu, familia na makundi yenye mahitaji maalum katika jamii iwe ni nyenzo muhimu kwa mustakabali wa maendeleo endelevu na jumuishi.
Waziri Mkuu amesema upatikanaji wa huduma za ustawi wa jamii ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita na sote tumeshuhudia dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuyawezesha makundi yenye uhitaji, kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kijamii.
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi baada ya kuwasili kwenye kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam kwa lengo la kufunga kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya chuo cha Ustawi wa Jamii, Desemba 18, 2023. Wa pili kulia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akipokea taarifa fupi kutoka kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipowasili kwenye kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kwa lengo la kufunga Kilele cha Maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii Desemba 18, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akimsikiliza Ofisa wa Kampuni ya Coca Cola Kwanza Victor Byemelwa alipotembalea banda la maonesho la Kampuni hiyo kabla ya kufunga Kilele cha Maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii Desemba 18, 2023. ( Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na viongozi wengine wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa kilele cha Maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii katika kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Desemba 18, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)