Featured Kitaifa

EWURA KUIMARISHA OFISI ZAKE ZA KANDA

Written by mzalendo

 

 

Kaimu Meneja wa Ofisi ya EWURA Kanda ya Magharibi, Mha. Walter Geofrey ( katikati) akifafanua jambo kwa Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt James Andilile( kushoto) wakati wa ziara ya kiongozi huyo mapema leo 6 Desemba 2023, kufuatilia maendeleo na utendaji wa ofisi hiyo. Kulia ni Mkurugenzi wa Fedha, Utawala na Rasilimaliwatu wa EWURA, Bwana Stanley Mahembe.

…………….

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt. James Andilile, amesema Mamlaka hiyo inaendelea kuimarisha ofisi zake kwenye ngazi ya Kanda ili kuwasogezea wananchi huduma, hali itakayowapunguzia muda na gharama na kuwawezesha kushiriki kwenye shughuli nyingine za uzalishaji.

Dkt. Andilile ameyasema hayo, leo 6 Desemba 2023, akiwa ziarani mkoani Tabora kukagua maendeleo na utendaji wa Ofisi ya EWURA Kanda ya Magharibi inayohudumia mikoa ya Tabora, Shinyanga, Katavi na Kigoma. Ametumia fursa hiyo pia kuwakumbusha wafanyakazi misingi ya utendaji na maadili ya utumishi wa umma.

“ Lengo la msingi la kuanzishwa ofisi hizi za Kanda ni kusogeza huduma karibu na wananchi.. tutaziongezea nguvu kwa kuleta haraka watalamu wenye weledi na vitendea kazi vya kutosha ili zihudumie watu wengi zaidi na kwa muda mfupi na huduma zote zipatikane kwenye ngazi ya Kanda,” alisema Dkt. Andilile.

Amewasihi watumishi kuhakikisha wanasimamia misingi ya haki, na kuepuka uonevu, ubaguzi na vitisho wanapohudumia wateja, na kusisitiza wazingatie maadili, heshima, sheria na taratibu ili kuleta ufanisi kwenye majukumu yao ya kila siku.

Kaimu Meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi, Mha. Walter Geofrey amesema ofisi yake imeendelea kutekeleza majukumu iliyokasimiwa kwa weledi na ufanisi tangu ilipoanzishwa tarehe 1 Julai 2023.

Huduma zitolewazo kwenye ofisi hiyo ni pamoja na leseni za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, vibali vya ujenzi na leseni za vituo vya mafuta, usajili wa watoa huduma kwenye kanzidata na usimamizi wa mamlaka za maji.

Awali, Mkurugenzi Mkuu huyo alimtembelea Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Batilda Salha Buriani ofisini kwake na kumshukuru kwa ushirikiano ambao amekuwa akiipatia EWURA kwenye utekelezaji wa majukumu yake mkoani hapo.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt James Andilile akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Ofisi za EWURA Kanda ya Magharibi, mjini Tabora leo 6 Desemba 2023. Ofisi hiyo inahudumia mikoa ya Tabora, Shinyanga, Katavi na Kigoma na imeanza shughuli zake tar 1 Julai 2023.

 

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt James Andilile ( kulia) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Dkt. Batilda Burian, alipomtembelea ofisini kwake leo 6 Desemba 2023 ili kumshukuru kwa ushirikiano anaoendelea kuuonesha kwenye utekelezaji wa shughuli za udhibiti wa huduma za nishati na maji katika mkoa huo.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt James Andilile ( kulia) akipokea asali kutoka kwa Kaimu Meneja wa Ofisi ya EWURA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Walter Geofrey, leo 6 Desemba 2023 wakati Dkt Andilile alipotembelea ofisi hiyo kufuatilia maendeleo na utendaji wake tangu kuanzishwa kwake Julai 1, 2023.

Kaimu Meneja wa Ofisi ya EWURA Kanda ya Magharibi, Mha. Walter Geofrey ( katikati) akifafanua jambo kwa Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt James Andilile( kushoto) wakati wa ziara ya kiongozi huyo mapema leo 6 Desemba 2023, kufuatilia maendeleo na utendaji wa ofisi hiyo. Kulia ni Mkurugenzi wa Fedha, Utawala na Rasilimaliwatu wa EWURA, Bwana Stanley Mahembe.

Picha ya pamoja ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt James Andilile (wa tano kutoka kulia) na baadhi ya watumishi wa EWURA baada ya kikao kazi na watumishi hao katika Ofisi za Kanda ya Magharibi, mjini Tabora leo 6 Desemba 2023.

About the author

mzalendo