Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI KAPINGA AWASHA MIRADI YA UMEME YA 20-BILIONI MOROGORO KUSINI

Written by mzalendo

Na.Issa Sabuni na Zuwena Msuya, Morogoro

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewasha umeme kwa mara ya kwanza katika vijiji viwili vya jimbo la Morogoro Kusini na kuwahamasisha wananchi kusuka umeme (Wiring) kwenye nyumba zao ili kuutumia katika kuleta maendeleo.

Naibu Waziri amesema hayo leo, Novemba 30, 2023 wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya umeme vijini na kuwasha Umeme Tayari (UMETA) katika Kata ya Mvuha wilaya ya Morogoro Vijijini.

Naibu Waziri Kapinga amewahamasisha wananchi hao kuunganisha umeme kwani serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika miradi lengo likiwa ni kuwainua kiuchumi.

Amewapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kutekeleza miradi ya umeme vijijini na kuwaahidi wananchi kuwa serikali itahakikisha kuwa vijiji vyote vinafikiwa ifikapo Juni 30, 2024.

Aidha amewashauri Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme nchini, TANESCO kuja na mpango mkakati utakaowawezesha wananchi wengi kusuka waya kwenye nyumba (wiring) kwa gharama nafuu.

“Serikali inatumia fedha nyingi kupeleka miradi ya umeme vijijini lakini wananchi wengi wanashindwa kuunganisha kutokana na kushindwa kumudu gharama za kusuka waya kwenye nyumba zao, tuone ni namna gani bora ya kuwasaidia” amesema.

Naibu Waziri Kapinga amewasha Umeme Tayari (Read Body) katika vijini vya Misaga na Kongwa katika Kata ya Mvuha ambapo wananchi waneishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwaletea umeme kwani umeongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na hivyo kujiongezea kipato.

Aidha Naibu Waziri Kapinga amesisitiza umuhimu wa wananchi kutunza mazingira na vyanzo vya maji ili kuwa na uhakika wa kuendelea kupatikana kwa umeme wa uhakika nchini hasa ikizingatiwa kuwa wananchi hao wanapakana na Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi, Jones Olotu amesema serikali imetoa kiasi cha shillingi Bilioni 20.5 kupeleka umeme vijijini katika jimbo la Morogoro Kusini.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kutumia umeme katika kujiletea maendeleo kwa kushiriki katika shughuli mbali mbali za kiuchumi (Uwekezaji).

“Jimbo la Morogoro Kusini lina vitongoji 447 kati hivyo 151 vina umeme na 296 ambapo kuna miradi miwili inaendelea ya kusambaza umeme kwenye vitongoji”.

Amesema Mhandisi Olotu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Morogoro Kusini, Mhe. Innocent Kalogeresi amewashauri REA kwa kusambaza umeme katika jimbo hilo ambapo kati ya vijiji 87, vijiji 82 tayari vina umeme huku vijiji vitano (5) vikiwa bado licha ya mkandarasi kuendelea na kazi ya kujenga miundombinu.

“Naipongeza REA kwa kuendelea kumsimamia mkandarasi (Kampuni ya Steg International Services) kwa kuendelea kusambaza umeme kwenye vitongoji 33 vya jimbo la Morogoro Kusini, vitongoji 25 tayari vina umeme huku vitongoji nane (8) vikiwa bado” Amekaririwa Mbunge Kalogolesi.

Ameishukuru serikali kwa kuhakikisha umeme umefika kwa wananchi wengi wa jimbo la Morogoro Kusini na kuiomba serikali kuona ni jinsi gani wananchi hao watanufaika na mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.

About the author

mzalendo