Featured Kitaifa

MHE. CHANDE AWAAGIZA CHUO CHA KODI KUFANYA TAFITI ZA MFUMO WA UKUSANYAJI WA KODI

Written by mzalendo
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande, akiwasitiza wahitimu kutumia ujuzi na maarifa waliyopata kwa faida ya Taifa wakati wa  Mahafali ya 16 ya Chuo Cha Kodi, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wahitimu wa Chuo Cha Kodi, wakisikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (hayupo pichani) wakati wa  Mahafali ya 16 ya Chuo cha Kodi, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande(katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi waliomaliza Shahada ya kwanza ya masuala ya kodi, wakati wa  Mahafali ya 16 ya Chuo Cha  Kodi, jijini Dar es Salaam.
 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha, Dar es Salaam)
Na: Josephine Majura na Scola Malinga WF – DSM
 
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amekiagiza Chuo cha Kodi kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitatoa suluhu ya changamoto zinazoukabili mfumo wa ukusanyaji kodi.
 
Ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya Kumi na Sita ya Chuo cha Kodi yaliyofanyika katika ukumbi wa Multipurpose.
Alisema tafiti hizo pia ziibue vyanzo vipya vya mapato, namna bora ya kudhibiti ukwepaji kodi pamoja na kufanya ulipaji kodi uwe rahisi na rafiki kwa kuzingatia teknolojia za kisasa zilizopo duniani.
 
Mhe. Chande alisema utozaji kodi na ukusanyaji wa mapato ni mambo yanayohusu wadau wengi, kuanzia watunga sera, watozaji kodi hadi walipakodi wenyewe.  
 
“Hivyo Mamlaka ya Mapato ina wajibu wa kukisaidia Chuo kupanua wigo wa kutoa mafunzo kwa wadau wengine ili nchi ipate wataalamu waadilifu wa kutosha wa masuala ya kodi na ipate walipakodi wazalendo ambao wanatambua wajibu wao wa kisheria wa kulipa kodi sahihi, kwa hiari na kwa wakati”, alisema Mhe. Chande.
 
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inathamini mchango ambao TRA inaoutoa katika juhudi za Serikali za kukuza mapato ya ndani na iko tayari kusaidia ili TRA ikiwezeshe Chuo kufanikisha majukumu na malengo yake.
 
Aidha, aliwasihi kuendelea kuimarisha ushirikiano na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili kuweza kubadilishana ujuzi, uzoefu na taarifa katika nyanja za forodha, kodi na tafiti mbalimbali za maeneo haya.
 
Mhe. Chande aliwapongeza wahitimu 508, ambao 293 ni wa kiume na 215 ni wa kike waliotunukiwa vyeti mbalimbali chuoni hapo na kuwasihi kutumia ujuzi na maarifa waliyopata kwa faida ya Taifa kwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa kodi au kwa kuwasaidia walipakodi watimize wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
 
Naye Mkuu wa Chuo cha Kodi, Prof. Isaya Jairo, alisema kuwa udahili kwa wanafunzi ambao ni wafanyakazi wa TRA umekuwa ukiongezeka kila mwaka tangu Chuo kipate Ithibati mwaka 2007 udahili wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania umeongezeka kutoka wanafunzi 974 mwaka 2008/2009 hadi kufikia wanafunzi 1,766 mwaka 2022/2023. 
 
Aliongeza kuwa Chuo kimendelea kushirikiana  na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, ambapo kimehuisha makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Kodi-International Bureau of Fiscal Documentation (IBFD), na kuendeleza ushirikiano na Mtandao wa Kimataifa wa Vyuo Vikuu vinavyotoa mafunzo ya Forodha.
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Cha Kodi, Dkt. Samwel Werema, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya elimu nchini na kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi.
 
Dkt. Werema alisema kuwa Katika muktadha huo, Chuo kitaendelea kubuni mafunzo mbalimbali kwa ajili ya wadau wa Mamlaka ambayo yanaendana na matarajio ya Serikali pamoja na mabadiliko ya kiuchumi Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.
 
Mahafali ya Kumi na Sita ya Chuo cha Kodi yaliyofanyika katika ukumbi wa Multipurpose, jijini Dar es Salaam, yamehudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Uledi Abbas Mussa, Kamishna Mkuu, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bw. Alphayo Kidata na viongozi mbalimbali wa Serikali na Wawakilishi wa Mamlaka ya Mapato  nchi jirani za Uganda na Burundi.

About the author

mzalendo