Featured Kitaifa

WAGANGA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA JUMUISHENI AFUA ZA KIFUA KIKUU NA UKOMA WAKATI WA AFUA NYINGINE

Written by mzalendo

Na. WAF – Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewaagiza Wanganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanajumuisha huduma za Kifua Kikuu na Ukoma kwenye shughuli zao wanazotekeleza ili kuongeza nguvu za kudhibiti Magonjwa hayo ifikapo Mwaka 2030.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Novemba 22, 2023 kwenye Mkutano mkuu wa Mwaka wa wataalamu wa Kifua kikuu na Ukoma uliofanyika Mkoani Dar es Salaam huku akisisitiza hatari ya kuambukizwa kwa Zaidi ya watu laki nne kwa mwaka.

“Naagiza waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya katika shughuli zenu mjumuishe Ukoma na Kifua Kikuu, nikienda kila mkoa nitaangalia ni namna gani waratibu wa mikoa na wilaya wanavyoshirikishwa kwenye shughuli zinazofanyika kwa rasilinali hizo hizo zilizopo”. Amesema Dkt. Mollel

Pia, Dkt. Mollel amesema kwa takwimu za Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Kifua kikuu na Ukoma, mgonjwa mmoja wa kifua kikuu ambaye hakupata matibabu anauwezo wa kuambukiza watu 15 hadi 20 kwa mwaka mmoja.

“Kutokana na wagonjwa 27,033 wenye maambukizi ya Kifua Kikuu kutopatikana kuanza tiba ya ugonjwa huo, kuna hatari ya watu 407,225 kuambukizwa kifua kikuu ndani ya mwaka mmoja” Amesema Dkt. Mollel

Akieleza mikakati ya kutokomeza Kifua kikuu nchini, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk John Jingu kupitia taarifa yake iliyosomwa na mwakilishi wake Catherine Joachim amesema Tanzania imewekewa lengo na Umoja wa Mataifa kutokomeza maambukizi ya kifua kikuu kufikia 2030

“Lengo ni asilimia 90 ya walioanzoshiwa dawa wawe wamepona hapa asilimia 95 tuliowaanzishia dawa wamepona, na tumepunguza vifo kwa asilimia 69 ya lengo la asilimia 90 tuliyojiwekea,”amesema.

Lengo la kujumuisha magonjwa ya Kifua kikuu na Ukoma kwenye shughuli zinazofanywa na waganga wakuu mikoa na wilaya ni kuendelea kuibua wagonjwa wa kifua kikuu ambao bado hawajaanza tiba.

About the author

mzalendo