Featured Kitaifa

DED APEWA WIKI MBILI KUWASILISHA MPANGO WA KUKAMILISHA UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI MLENGE

Written by mzalendo

Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde akielekeza kukamilisha ujenzi wa Shule ya Sekondari Mlenge iliyopo Kitongoji cha Mbugani Kijiji cha Magombwe ili kuwawezesha wanafunzi wa eneo hilo kupata elimu bora.

Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde (mwenye suti) akikagua moja ya jengo katika Shule ya Sekondari Mlenge iliyopo Kitongoji cha Mbugani Kijiji cha Magombwe.

Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde (mwenye suti) akielekeza jambo wakati akikagua moja ya jengo katika Shule ya Sekondari Mlenge iliyopo Kitongoji cha Mbugani Kijiji cha Magombwe.

Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde (mwenye suti) akielekea kukagua ujenzi wa Shule ya Sekondari Mlenge iliyopo Kitongoji cha Mbugani Kijiji cha Magombwe.

Mwonekano wa majengo ambayo hayajakamilika katika Shule ya Sekondari Mlenge iliyopo Kitongoji cha Mbugani Kijiji cha Magombwe.

Na: James Mwanamyoto 

Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles Msonde amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini Bw. Bashir Muhoja ndani ya wiki mbili kuhakikisha amewasilisha mpango mkakati wa namna atakavyokamilisha ujenzi wa Shule ya Sekondari Mlenge iliyopo Kitongoji cha Mbugani Kijiji cha Magombwe ili kuwawezesha wanafunzi wa eneo hilo kupata elimu katika mazingira mazuri.

Dkt. Msonde ametoa maelekezo hayo mapema leo, mara baada ya kuitembelea shule hiyo inayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP kwa lengo la kukagua na kujionea maendeleo ya ujenzi.

Dkt. Msonde amesema kuna baadhi ya maeneo ambayo shule zilizojengwa kupitia mradi wa SEQUIP hazijakamilika lakini si kwa kiwango cha chini kama cha Shule ya Sekondari Mlenge, kwani katika maeneo mengine ujenzi wa shule umekamilika kila jengo isipokuwa miundombinu ya ndani ya maabara, au rangi haijapigwa.

“DED hakikisha majengo haya yanakamilika mapema iwezekanavyo na ndani ya wiki mbili uwasilishe kwa KM OR TAMISEMI mpango mkakati wa namna ya ujenzi wa shule hii utakavyokamishwa,” Dkt. Msonde amesisitiza.

Dkt. Msonde ameongeza kuwa, Serikali inataka mwaka huu wa fedha ukiisha na shule zote ziwe zimekamilika ili kutimiza lengo lake la kuboresha miundombinu ya elimu itakayokuwa na tija kwa wanafunzi ambao wakielimika wawe katika nafasi nzuri ya kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Dkt. Msonde amefafanua kuwa, kitendo cha kutokamilisha ujenzi wa shule hiyo ni ishara ya kupuuza maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI ambayo aliyatoa mwaka jana akiwata Wakurugenzi kukamilisha kwa wakati ujenzi wa shule ili kuunga mkono kwa vitendo dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Serikali kupitia Mradi wa SEQUIP ilitoa shilingi milioni 470 kwa ajili ya kujenga Shule ya Sekondari Mlenge ambayo ipo katika kata ya Mlenge ambayo haikuwa na Shule ya Sekondari hivyo kuwalazimu wanafunzi waliofaulu kutoka shule za msingi Kisanga, Kinyika, Magombwe na Isele kupangiwa Shule ya Sekondari Pawaga ambayo imekuwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi.

 

About the author

mzalendo