Featured Kitaifa

WAZIRI BASHUNGWA AWAFUNDA MAMENEJA TANROADS, ASISITIZA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA

Written by mzalendo

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akizungumza na Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), wa mikoa yote nchini katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akisisitiza jambo kwa Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), wa mikoa yote nchini (hawapo pichani), katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (kulia), akijadiliana jambo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Eng. Aisha Amour (kushoto), wakati wa kikao cha Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), wa mikoa yote nchini kilichofanyika jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Mohamed Besta, akitoa taarifa ya utekelezaji wa Wakala huo katika kikao kazi kilichowakutanisha Viongozi wakuu wa Wizara na Mameneja wa Wakala huo kutoka mikoa yote nchini, jijini Dodoma.

Sehemu ya wajumbe wa Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) wakiwa katika kikao kazi ilichowakutanisha Viongozi wakuu wa Wizara ya Ujenzi na Mameneja hao kutoka mikoa yote nchini, jijini Dodoma.

PICHA NA W-Ujenzi

……………………..

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amewataka Mameneja wa Mikoa wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuhakikisha wanaendelea na mapambano na dhidi ya rushwa katika maeneo yao ya kazi na nje ya kazi ili kujenga taswira nzuri kwa Wakala huo na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha Mamemeja hao, tarehe 17 Novemba, jijini Dodoma, Waziri Bashungwa amesisitiza Mameneja hao kuendelea na Mapambano dhidi ya rushwa ni bila kuchoka kwenye sekta ya ujenzi kuanzia manunuzi na usimamizi wa miradi ya ujenzi.

Bashungwa amewata kuhakikisha kuwa wanaripoti  kwake au katika mamlaka husika endapo watahisi kuna viashiria vyovyote vya rushwa mapema ili hatua stahiki kuchukuliwa kwa wakati.

“Ninyi ni sehemu ya ulinzi wa kusaidia kupambana na rushwa, msisite kuendelea kupambana na suala hili kwa pamoja kuanzia katika hatua za manunuzi hadi kwenye utekelezaji wa mikataba, Mheshimiwa Rais anataka kuona mnafanya weledi mkubwa katika utekelezaji wa miradi, kufanya hivi mtasaidia  kulinda rasilimali za serikali zinazopotea kutokana na kukosa uzalendo kwa baadhi ya watu”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amewataka Mamemeneja hao kuhakikisha hatua kwa mujibu wa sheria kwa yeyote aliyevamia maeneo ya hifadhi ya barabara na kuendelea kusimamia kwenye maeneo yao kuhakikisha kuwa sheria hiyo haivunjwi.

Bashungwa amewataka Mameneja hao kuwa na tamaduni ya kuwajengea uwezo watumishi wao ili kuongeza ufanisi na tija kwa Taasisi hiyo  pamoja na Taifa kwa ujumla samambamba na urithishaji wa ujuzi kwa watumishi walio chini yao kwa lengo la kuwekeza katika vizazi vya sasa na vijavyo  .

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya,  amewapongeza Mameneja hao kwa kazi kubwa wanazofanya katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini  na kusisitiza kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa viongozi wa serikali waliopo katika maeneo yao.

 

“Niwapongeze kwa ushirikiano mnaoutoa kwa viongozi mbalimbali wanapowaita katika mikutano ya kiutendaji au kuwatembelea katika miradi yenu kujua hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi, utaratibu huu ni mzuri nawasihi muendelee nao,  hii inaonyesha ni jinsi gani mnaungana nao katika kuhakikisha taarifa za utekelezaji wa miradi zinafahamika kwa wote”, amesema Kasekenya.

Kasekenya amewataka TANROADS kuandaa mkakati wa kuboresha maeneo korofi ambayo yatapewa kipaumbele ili utekelezaji wake uweze kufanyika haraka na kuweza kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Naye, Katibu wa Wizara hiyo, Balozi, Mhandisi Aisha Amour, ameishukuru Wizara ya fedha kwa kuendelea kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 70 kila mwezi kwa ajili ya kulipa madeni ya wakandarasi ambapo kati ya fedha hizo Bil. 20 ni kwa ajili ya wakandarasi wa nje  na Bil.50 ni kwa ajili ya wakandarasi wa ndani.

“Tunaishukuru serikali kwa kuendelea kutugawia  kiasi hiki cha fedha ili kupunguza mzigo wa madeni, tunaamini hali hii ikiendelea madeni ya makandarasi yatakuwa sio changamoto tena”, amesema Balozi Amour.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa Wakala huo, Mtendaji Mkuu wa TANOROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema kuwa Wakala utahakikisha unayafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Waziri huyo ikiwemo kuandaa  mpango maalum wa pamoja wa uwekaji wa taa za barabarani katika mikoa yote nchini.

Kikao kazi hicho chenye lengo la kuimarisha ushirikiano na kuboresha utendaji kwa Wakala huo kimeshirikisha viongozi wakuu wa Wizara na Mameneja wa Wakala huo kutoka mikoa yote nchini. 

About the author

mzalendo