Addis Ababa, Ethiopia
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Mashariki na Kusina mwa Afrika Dkt. Victoria Kwakwa ameitaja na ameipongeza Tanzania kuwa kinara na mfano katika utekelezaji wa programu ya uendelevu wa huduma ya maji na usafi wa mazingira vijijini Mashariki na Kusini mwa Afrika na Duniani kwa kutumumia utaratibu wa malipo kwa matokeo yaani Programme for Results (PforR) ambayo inatekelezwa katika nchi zaidi ya 50 na kufadhiliwa na Benki ya Dunia.
Akizungumza na Waziri wa Fedha Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba pamoja na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso, Makamu wa Rais Kwakwa amesema Tanzania ni mfano bora katika utekelezaji wa Programu ya PforR na ameiomba itoe uzoefu wa mafanikio yake kwa nchi zaidi ya 23 kutoka kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika zinazoshiriki mkutano wa maji na usafi wa mazingira (WASH Leadership Summit).
Awali Tanzania ilipata Dola za Kimarekani milioni 350 katika miaka mitano lakini ndani ya miaka mitatu ya kwanza ilikuwa imefikisha maji kwa zaidi ya watu wapya millioni 4.7 vijijini katika mikoa 17. Kufuatia mafanikio hayo, kulingana na matokeo hayo, Benki ya Dunia imeiongezea Tanzania Dola za Marekani milioni 300 na hivyo kupanua wigo wa utekelezaji kufikia mikoa 25. Kwa sasa shillingi milioni 970 zimepelekwa katika Halmashauri zote kwa ajili ya kuanza utekelezaji.
Aidha, mafanikio haya yamefungua rasmi milango uendelevu ya programu hii ambayo inafikia ukomo Julai 2025. Kufuatia hoja ya Tanzania ya kuwa na PforR Awamu ya Pili, Benki ya Dunia imeonesha utayari wa kuwa na PforR Awamu ya pili katika kipindi cha 2025-2030.
Serikali kupitia programu hii ya lipa kwa matokeo (PforR) imetekeleza zaidi ya miradi ya maji 1,500 ambayo imekamilika na inatoa huduma.