Featured Kitaifa

SERIKALI YAJA NA MBINU KUDHIBITI MAAMBUKIZI YA VVU KWA KUNDI LA VIJANA

Written by mzalendo

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Novemba 14,2023 jijini Dodoma kuelekea maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yanayotarajia kuadhimishwa Disemba Mosi Mwaka huu Mkoani Morogoro.

Makamu Mwenyekiti wa Nacopha wa Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na VVU (NACOPHA), Bw, Emanuel Reuben Msinga .akifafanua  wakati wa Mkutano kuelekea maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yanayotarajia kuadhimishwa Disemba Mosi Mwaka huu Mkoani Morogoro.

Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) na Watendaji wa TACAIDS wakifuatilia Mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama,(hayupo pichani) akizungumza na waandishi wa habari  kuelekea maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yanayotarajia kuadhimishwa Disemba Mosi Mwaka huu Mkoani Morogoro.

Na.Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI  wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Utaribu, Jenista Mhagama,amesema takwimu za sasa kuhusu hali ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) nchini, zinaonyesha kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanachangia maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 40.
Waziri  Mhagama, ameyabainisha hayo leo Novemba 14,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Morogoro.
Waziri Mhagama amesema kuwa jitihada zimekuwa zikielekezwa zaidi kuhakikisha kundi hilo linaondoka katika mstari huo wa maambukizi.
“Maadhimisho ya mwaka huu yatatoa kipaumbele kwa vijana. Tutatoa nafasi ya kuwasikiliza, waeleze yakwao lakini pia watakutana na viongozi wa dini, viongozi wa kijamii wakiwemo machifu,” amesema Waziri Mhagama
Mhe,Mhagama amesema  katika maadhimisho hayo takwimu mpya kuhusu hali ya maambukizi ya VVU na Ukimwi, zitatangazwa rasmi baada ya utafiti wake kukamilika ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
”Huduma za VVU na Ukimwi zimeendelea kutolewa kwa kiwango kikubwa nchini huku akitoa msisitizo kwa wanaume kujitokeza kupima afya zao kwani bado katika tafiti tano kuhusu hali ya maambukizi ya VVU nchini, zimebaini wanaume bado wamekuwa wazito kwenda kupima.”amesisitiza 
Kuhusu utoaji dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARVs) amesema dawa hizo zimekuwa zikitolewa kwa kiwango kikubwa kwa lengo la nchi kufikia mkakati wa dunia wa 95 tatu.
“Malengo hayo ya kidunia ya 95 tatu kwanza ni kuhakikisha asilimia 95 ya wananchi wote watambue hali zao hususan wale wenye maambukizi ya VVU, asilimia 95 ya wenye VVU wapate dawa za kufubaza virusi na asilimia 95 ya wenye maambukizi wawe wamefubaza virusi vya VVU,” amesema

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na VVU (NACOPHA) Bw. Emmanuel  Msinga amesema kuwa  katika kuhakikisha vijana wanashiriki zaidi kutambua afya zao, baraza hilo limeandaa program mbalimbali za vijana kuhusu VVU.

”Kkupitia program hizo, vikundi vya vijana wanaoishi na VVU wamekuwa wakitoa elimu kwa vijana wenzao kuhamasisha kujitokeza kupima VVU ili kufahamu hali zao.”amesema Bw.Msinga
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Dk. Jerome Kamwela, amesema suala la wanaume kutojitokeza kwa wingi kupima VVU limekuwa likijirudia katika tafiti zote tano zilizofanyika nchini.
”Wanaume wenye maambukizi ya VVU wamekuwa wakiongoza kufariki dunia kuliko wanawake kwa sababu ya kutojitokeza mapema kupima afya zao na kuanza kutumia dawa za kufubaza VVU pindi wakibainika kupata maambukizi.”amesema Dk.Kamwela

Kauli Mbiu kwa Maadhisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa mwaka huu inasema; “JAMII IONGOZE KUTOKOMZEA UKIMWI.”

About the author

mzalendo