Featured Kitaifa

HAKIKISHENI TAKWIMU SAHIHI ZINAPATIKANA KUSAIDIA MIPANGO YA MAENDELEO YA SEKTA YA AFYA

Written by mzalendo

Na. WAF – Morogoro

Waratibu wa Mfumo wa Takwimu wa Taarifa za Uendeshaji wa Huduma za Afya Nchini (HMIS) wametakiwa kuhakikisha ukusanyaji wa takwimu kwa kutumia mifumo ya kielektroniki unafikia vituo vyote vya kutolea huduma za Afya.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema hayo leo Novemba 13, 2023 wakati akifungua mkutano wa mwaka wa waratibu wa takwimu za Afya Mkoani Morogoro.

“Hakikisheni mnaimarisha ustadi wa kuchambua takwimu na kufikisha matokeo kwa wananchi kwa wakati ili takwimu sahihi zitumike katika Mipango mbalimbali ya Maendeleo na tunatakiwa kuwa na mifumo michache ya takwimu inayosomana ili kupunguza gharama kwa Serikali.” Amesema Dkt. Jingu

Aidha, Dkt. Jingu amesema kuwa takwimu zote zinazokusanywa nje ya Mfumo wa DHIS2 kama vile GoT- HoMIS, eMR, VIMS-BID, CTC ziwe zinapatikana katika mfumo wa DHIS2 ili kuwezesha Sekta ya Afya kupata viashiria vya Kitaifa na kusisitiza uimarishwaji wa vitabu vya kukusanyia takwimu hizo.

“Tukiwa tunaendelea kuimarisha mifumo ya kielektroniki lakini pia hakikisheni vitabu vyote vya kukusanyia takwimu vinajazwa kwa usahihi kwa kuwa takwimu sahihi zinasaidia kujua kazi zetu tulizokabidhiwa na majukumu kama tumeyafanya kwa usahihi.” Amesema Dkt. Jingu

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema Upatikanaji sahihi wa takwimu utawezesha uwepo na upatikanaji wa dawa kwa kipimo sahihi kulingana na uhitaji wa maeneo husika.

“Sekta ya Afya inaendelea kuwekeza katika upatikanaji wa huduma kwa Jamii ambapo elimu sahihi ya Kinga itakuwa inatolewa pamoja na utambuzi wa mapema wa magonjwa mbalimbali, hivyo takwimu sahihi na zinazotolewa kwa wakati ni nguzo ya mafanikio ya juhudi hizi.” Amesema Prof. Nagu.

Nae Kaimu Mkurugenzi Ufuatiliaji na tathmini kutoka Wizara ya Afya, Claud J. Kumalija amesema malengo ya kikao ni kufanya tathmini ya hali ya sasa ya takwimu za Afya na kuazimia, kujadili bunifu mpya zitakazo lenga kuwezesha mifumo ya takwimu za Afya kusomana kupitia mfumo wa DHIS2 na kuwezesha takwimu kuwafikia wahitaji kwa njia rahisi ya simu za mikononi ili takwimu za Afya ziweze kutumika katika mipango na maamuzi ya Sekta ya Afya nchini.

About the author

mzalendo