Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU ATETA NA MAKONDA

Written by mzalendo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi, Paul Makonda kabla ya mazungumzo yao ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi, Paul Makonda, ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Novemba 2, 2023. (Picha na Ofisi ya Wziri Mkuu)

*Asema ni kiongozi mchapakazi na mtiifu, Chama kina matumaini makubwa

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi Paul Makonda amesema CCM haina shaka na utendaji kazi wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwani ni kiongozi mchapakazi na mtiifu.

“…Katika utendaji wa kazi sisi upande wa Chama tuna matumaini makubwa na uwajibikaji na uaminifu wa Waziri wetu Mkuu Kassim Majaliwa, tumemuona katika maeneo mengi akisimamia shughuli mbalimbali za Serikali na nilipotoa agizo la Chama kwa Waziri Mkuu nilitaka agizo hilo lifike kwa mtu anayeweza kuleta matokeo chanya kwa Chama.”

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi amesema lengo la CCM chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Serikali inatimiza kile ambacho imepewa kukifanya kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi, hivyo wana matumaini makubwa na utendaji kazi wa Mheshimiwa Majaliwa.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Novemba 2, 2023) alipokwenda ofisini kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma. Amesema lengo la Chama ni kuhakikisha ndoto ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wote hususani wanyonge inafikiwa.

Amesema Waziri Mkuu ni mtendaji mtiifu, mwaminifu na kwamba maelezo yaliyotolewa kwake na CCM kuhusu kushughulikia migogoro ya ardhi tayari ameyapokea na ameanza kuyatekeleza. “Nina imani hata miezi sita tuliyompa inawezekana akatumia hata miezi mitatu tukapata ripoti.”

Kadhalika, Makonda amesema Chama kimemwagiza Waziri Mkuu kuwachukulia hatua wote ambao wataonekana kukwamisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya Serikali. “Yeyote ambaye anabainika kufanya ubadhirifu wa mali za umma na Waziri Mkuu akabaini achukue hatua mara moja na Chama tumempa baraka zote.”

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema Serikali imepokea maelekezo ya Chama na kwamba itaendelea kuyafanyia kazi na kuhakikisha migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini inaendelea kushughulikiwa.

Akizungumzia kuhusu suala la udhibiti wa fedha za umma, Mheshimiwa Majaliwa amesema serikali itaendelea kulisimamia jukumu hilo ili fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo zitumike ipasavyo na katika viwango vya ubora vinavyotakiwa. 

About the author

mzalendo