Featured Kitaifa

UJENZI WA JENGO JIPYA OFISI ZA WIZARA YA ELIMU WAFIKIA 80%

Written by mzalendo

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo ameielekeza Kampuni ya China ya CRJE inayotekeleza mradi wa ujenzi wa majengo ya Wizara ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia kuongeza nguvu kazi na muda wa kazi ili kuhakikisha jengo hilo linakabidhiwa ifikapo Disemba 15, 2023 kulingana na makubaliano ya mkataba.

Prof. Nombo ametoa maelekezo hayo Novemba Mosi, 2023 wakati alipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo jipya la Ofisi za Wizara hiyo lililopo katika Mji wa kiserikali Mtumba ili kujionea maendeleo ya mradi huo.

“Jengo limefikia asilimia 80, kwa hatua hii Mkandarasi amejitajidi, na amenihakikishia kwamba watakabidhi jengo kwa wakati kulingana na makubaliano ya mkataba” alisema Prof. Nombo

Aidha Katibu Mkuu huyo ameishukuru kampuni ya ABBEC kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi ambayo ndio Mshauri Elekezi wa mradi wa ujenzi huo kwa kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Mkandarasi na kwamba hali hiyo itasaidia kutekeleza mradi kwa ufanisi na kwa wakati.

“Nimeona kazi ndani ya jengo zikiendelea, ikiwemo ya kuweka _partition_, kuweka miundombinu ya AC pamoja na kupaka rangi kwenye vyumba, lakini wanahitajika kuongeza jitihada zaidi kuhakikisha jengo linakamilika kwa wakati uliopangwa” alisema Prof. Nombo.

Ameongoza kuwa wakati kazi zingine za nje ya jengo zikiendelea, Wizara itawasiliana na Mamlaka nyingine ili kuhakikisha miundombinu mbalimbali katika jengo hilo nayo inakamilika kwa wakati.

Akizungumza kufuatia ziara hiyo, Meneja wa mradi wa Kampuni ya China ya CRJE Li Yang ameishukuru serikali kuwapatia nafasi ya kutekeleza mradi huo, ambapo ameahidi kukamilisha ujenzi wa jengo hilo na kukabidhi kwa wakati.

Kwa upande wake Mhandisi Renatus Dominic kutoka Kampuni ya ABBEC ya Chuo Kikuu cha Ardhi ambayo ndio Mshauri Elekezi wa mradi huo, amemhakikishia Katibu Mkuu Wizara ya Elimu kwamba watashirikiana kikamilifu na Mkandarasi waweze kukabidhi jengo kwa muda uliopangwa.

“Tunaishukuru ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu kutembelea mradi wa ujenzi kuona kinachoendelea mpaka sasa, hatua hii imetuhamasisha sana, tunamuahidi kuendeleza Ushirikiano na Mkandarasi aweze kukamilisha ujenzi kwa wakati uliopangwa” alisema Mhandisi Dominic

Akifafanua kazi zinazoendelea ndani ya jengo, Mhandisi Dominic amesema ni pamoja na kupaka rangi na kuweka miundombinu ya huduma wezeshi za jengo.

Pia ameushukuru Uongozi mzima unao simamia mradi, kupitia kampuni ya ABBEC pamoja na Watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu ambao wameshirikiana katika kutekeleza mradi wa ujenzi huo.

About the author

mzalendo