Featured Kitaifa

WATANO WASHIKILIWA KWA KUTOROSHA MADINI YA DHAHABU.

Written by mzalendo

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na kikosi kazi cha tume ya madini, linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kutorosha madini na kufanya biashara ya madini bila kuwa na kibali. Watuhumiwa waliokamatwa ni 1. Masunga Kidishi [43] 2. Timoth Simbu [26] 3. Ngunje Ideshi [41] 4. Ester John [25] na 5. Baraka Silwani [28] wote wafanyabiashara na wakazi wa Chokaa Wilaya ya Chunya.

Watuhumiwa walikamatwa Oktoba 26, 2023 huko Mtaa wa kibaoni wilayani Chunya wakiwa na madini aina ya dhahabu vipande 160 vyenye uzito wa gramu 6,933.6 wakiwa hawana nyaraka “transport permit” wakiwa wanatorosha madini hayo kwenda kuuza nje ya mfumo wa soko la dhahabu. Wataalamu kutoka Wizara ya Madini wanaendelea na uchunguzi ili kujua thamani halisi ya madini hayo. 

Aidha dhahabu vipande 145 vilipatikana baada ya kupekua kwenye makazi ya mtuhumiwa Ngunje Ideshi. Awali kabla ya kukamatwa vipande hivyo vilikamatwa vipande 15 vya dhahabu kwenye Gari T.796 DTT IST iliyokuwa na watuhumiwa Timoth Simbu na Ngunje Kidishi. Watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

RAIA 11 WA ETHIOPIA WAKAMATWA KWA KUINGIA NCHINI BILA KIBALI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia raia 11 wa Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila kuwa na kibali. Watuhumiwa walikamatwa Oktoba 27, 2023 huko eneo la Igawa wilaya ya Mbarali katika barabara kuu ya Mbeya – Njombe wakati Askari Polisi wakiwa doria.

Watuhumiwa waliokamatwa ni:- 1. Mulatoto Amdado, 2. Nugushi Handibal, 3. Aulosy Segea, 4. Takatary Mwanjiso, 5. Goodso Bekere, 6. Lamborn Ondose, 7. Ndale Kermah, 8. Kibiruh Tamrah, 9. Tafasah Alarm, 10. Mestin Tasfay na 11. Chalu Ababa wote wanaume.

Watuhumiwa walikuwa wakisafirishwa kwa kutumia Gari T.732 CRB Toyota Mark X rangi nyeupe. Dereva wa Gari aitwaye Frank Makunde [38] mkazi wa Makambako Mkoa wa Njombe amekamatwa kwa hatua zaidi za kisheria. Ufuatiliaji zaidi unaendelea ili kuwabaini wasafirishaji wengine pamoja na mmiliki wa Gari.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wafanyabiashara ya madini kufuata utaratibu wa kuuza na kununua madini katika masoko yaliyopo kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu. Aidha, Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi kuacha mara moja kujihusisha na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu [wahamiaji haramu] kwani ni kinyume cha sheria, watakamatwa, kufungwa gerezani na mali zao kutaifishwa hivyo ni vyema wakatafuta kazi nyingine za kufanya ili kujipatia kipato halali.

Imetolewa na:

BENJAMIN KUZAGA – ACP

Kamanda wa Polisi,

Mkoa wa Mbeya.

About the author

mzalendo