Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU AFUNGUA MKUTANO WA CHAMA CHA MENEJIMENTI YA KUMBUKUMBU

Written by mzalendo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Mkutano Mkuu wa 11 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma

Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa 11 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA)wakimsikiliza  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua mkutano huo kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea zawadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simabachawe iliyotolewa na Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) ikiwa ni shukurani kwa Rais kutokana na mchango wake mkubwa katika kuiheshimisha taaluma ya kutunza kumbukumbu na nyaraka nchinil. Waziri Mkuu alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa 11 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Oktoba 27, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

……...

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua Mkutano Mkuu wa 11 wa Kitaaluma wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA) ambapo amewataka watunza kumbukumbu na nyaraka wazingatie miiko ya taaluma yao hususan utunzaji siri za Serikali na kufuata utaratibu rasmi wa utoaji taarifa.

“Hakikisheni mnadhibiti matukio yanayokiuka taratibu ikiwemo kutumia mifumo rasmi katika kusafirisha na kutuma nyaraka badala ya kutumia njia zisizo sahihi. Ninasisitiza kila mmoja azingatie wajibu wa kutunza nyaraka na kudhibiti utupaji ovyo wa nyaraka na kusababisha kukutwa sokoni zikifungiwa bidhaa au kuachwa zikizagaa na kukutwa katika mikono isiyo sahihi.”

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Ijumaa, Oktoba 27, 2023) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa TRAMPA katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza wadhibiti uvujaji wa siri za Serikali.

“Wanachama wa TRAMPA zingatieni misingi ya kuanzishwa chama chenu. Hiki ni chombo kinachowakilisha taaluma kwenye taasisi mbalimbali nchini na siyo chama cha kisiasa hivyo fanyeni yaliyo ya kitaaluma kama alivyowaasa Mlezi wa Chama chenu ambaye anataka kuona chama kikiendelea vizuri.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kila mtunza kumbukumbu awe msaada na mlinzi wa mwenzake ili kudhibiti upotevu wa nyaraka na majalada yenye taarifa muhimu. “Toeni taarifa kwa mamlaka kuhusu uwepo wa viashiria vya baadhi ya maafisa kumbukumbu wasio na maadili wanaosababisha upotevu wa nyaraka.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesisitiza Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma iweke mpango mahsusi wa kupunguza uhaba wa watunza kumbukumbu ikiwa ni pamoja na kuandaa kanzidata, wabainishe mahitaji na kuharakisha utoaji wa vibali vya ajira ya kada za watunza kumbukumbu kwa idara ambazo tayari zimeshatenga ikama ya watumishi wa kada hiyo.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Maafisa Masuhuli wasimamie Ofisi za Masijala kwa kudhibiti vitendo vya kufanya ofisi hizo kuwa dampo au sehemu ya chakula. “Kila Afisa Masuhuli asimamie vizuri taratibu za kutunza au kuhifadhi nyaraka Pia yapo mazoea ya baadhi ya Viongozi kuzifanya Ofisi za Masijala kutumika kwa kula chakula. Ofisi ziwe na maeneo ya chakula.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada za makusudi kuimarisha sekta ya umma kwa kufanya maboresho mbalimbali ili kuiwezesha sekta hiyo ikidhi matarajio ya umma. “Jitihada zote hizo haziwezi kuwa na manufaa iwapo hakuna mifumo madhubuti ya kuhifadhi taarifa.”

Ametaja maboresho mengine kuwa ni pamoja na kuziboresha masijala za Serikali kwa kuziwekea vifaa na vitendea kazi vyenye viwango ili kukidhi mahitaji ya sasa kuharakisha utoaji huduma kwa wadau na wananchi kwa ujumla na kutambua, kukusanya na kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka muhimu katika kuhifadhi historia na urithi andishi wa nchi yetu kwa matumizi ya sasa na kwa vizazi vijavyo.

About the author

mzalendo