Featured Kitaifa

RAIS SAMIA KUWA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA MIKA 59 YA UHURU WA ZAMBIA

Written by mzalendo

Dar es Salaam 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia  Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi katika Sherehe za  Maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa Jamhuri ya Zambia zinazotarajiwa  kufanyika tarehe 24 Oktoba 2023 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali  kutoka ndani na nje ya bara la Afrika. 

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia amealikwa kuwa mgeni  rasmi katika sherehe hizo na Rais wa Jamhuri ya Zambia Mheshimiwa  Hakainde Hichilema. 

Mheshimiwa Dkt. Samia pia amealikwa kufanya Ziara ya Kitaifa nchini  Zambia kuanzia tarehe 23 – 25 Oktoba 2023 ambapo pamoja na mambo  mengine, atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kongamano la Biashara  kati ya wafanyabishara wa Tanzania na Zambia. 

“Ziara hii ni ya kwanza ya Kitaifa ya Mheshimiwa Rais kufanya nchini Zambia  tangu alipohudhuria uapisho wa Rais Haichilema mwaka 2022, itakumbukwa kuwa  Tanzania na Zambia zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao  umejengwa na misingi ya kindugu,” alisema Waziri Makamba. 

Mhe. Waziri Makamba amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia pia  amepewa heshima ya kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Zambia tarehe 25  Oktoba, 2023 na anakuwa kiongozi mashuhuri wa wanne kuhutubia Bunge hilo. 

“Mhe. Rais katika ziara hii amepewa heshima kubwa ya kuhutubua Bunge la  Jamhuri ya Zambia, hii ni heshima kubwa na ya kipekee kwa Mheshimiwa Rais Dkt.  Samia kwani anakuwa mgeni mashuhuri wa nne kuhutubia Bunge la Jamhuri ya  Zambia tangu mwaka 2012,” Alisema Waziri Makamba 

Waziri Makamba aliongeza kuwa ziara hiyo inalenga kudumisha  ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Zambia katika maeneo ya kimkakati  ya sekta za uchukuzi, nishati, biashara na miundombinu na kuongeza kuwa  katika ziara hiyo Mhesimiwa Rais Dkt. Samia na Mwenyeji wake watajadili  namna ya kuboresha miundombinu inayomilikiwa kwa pamoja kati ya  Tanzania na Zambia ikiwemo Bomba la Mafuta la TAZAMA, Reli ya  TAZARA na barabara ya TANZAM. 

Aidha, malengo mengine ya ziara hiyo ni pamoja na kuweka mazingira  wezeshi na rafiki kwa wafanyabiasha na wasafirishaji ili waweze kuendesha  shughuli zao kwa urahisi, kuibua fursa mpya za ushirikiano na kuieleza  jumuiya ya wafanyabiashara Zambia kuhusu maboresho yaliyofanyika  katika bandari ya Dar es Salaam. 

Akielezea kuhusu urari wa biashara kati ya Tanzania na Zambia, Mhe.  Waziri Makamba amesema mwenendo wa ukuaji wa Biashara kati ya  Tanzania na Zambia umeendelea kuongezeka kwa miaka ya hivi karibuni  ambapo mwaka 2016 Tanzania iliuza nchini Zambia bidhaa zenye thamani  ya shilingi bilioni 70,815.40 na kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia shilingi  bilioni 183,648.5 kwa mwaka 2022.  

About the author

mzalendo