Featured Kitaifa

RAIS SAMIA APEWA TUZO MTETEZI WA HAKI ZA BINADAMU

Written by mzalendo

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunikiwa tuzo ya Mtetezi wa Kwanza wa Haki za Binadamu na Mtandao wa Taifa wa Watetezi wa Haki za Binadamu.

Tuzo hiyo imetolewa leo Oktoba 21, 2023 katika Kituo Cha Mikutano Cha Kimataifa cha Arusha (AICC) wakati wa Kikao Cha 77 cha Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kinachoendelea jijini Arusha.

Akizungumza wakati akipokea tuzo hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana amesema, “nipo hapa kwa heshima na taadhima kupokea tuzo ya mwanamke kiongozi shujaa, mwanamke kiongozi mchapakazi, mwanamke kiongozi mjasiri, mwanamke kiongozi mtetezi wa haki za binadamu na watu, mwanamke kiongozi mtoto wa afrika, mwelewa na mleta maendeleo”.

Aidha amesema kuwa, Tanzania imeendelea kusimama na kutekeleza mipango mbalimbali ya Kitaifa, Kikanda na Kidunia katika kuhifadhi, kukuza, kulinda na kutetea haki za binadamu nchini.

Dkt Chana ameongeza kuwa, katika kipindi cha Awamu ya Sita kinachoongozwa na Rais Samia kumekuwa na kasi katika kuleta maendeleo na kuwezesha mifumo ya upatikanaji haki kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo utoaji wa haki huru na uhuru wa kujieleza, uhuru wa imani, uhakika wa chakula na haki nyingine ikiwemo uwezeshaji vijana kujiajiri na kuwezesha wanawake.

“Kwa upande wa Wizara ya Katiba na Sheria sasa tupo kwenye usajili wa watoto chini ya umri wa miaka mitano wanapata usajili wa vyeti vya kuzaliwa bure, msaada wa kisheria ambao unaitwa Dkt. Samia Legal Aid kwa wote lakini mahakamani sheria zetu tumeanza kutumia lugha ya Kiswahili ili kuwezesha watu wote kuelewa,” amefafanua.

Vilevile amebainisha kuwa, katika kipindi hiki cha Awamu ya Sita kumekuwa na ongezeko la wanawake kwenye vyombo vya utoaji wa maamuzi ikiwemo kwenye mahakama ambapo kuna majaji kuanzia Mahakama ya Rufaa hadi Mahakama Kuu lakini pia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liloongozwa na Spika wa Bunge mwanamke.

Awali wakati akiwasilisha mada kuhusu Itifaki ya Mkataba wa Haki za Binadamu wa Maputo (Maputo Protocol) kuhusu changamoto za utekelezaji wake, uhuishaji wake na utoaji wa taarifa aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mwakilishi wa Bunge, Mhe. Prof. Palamagamba Aidan Mwaluko Kabudi amebainisha kuwa, Serikali ya Jumhuri ya Muungano Tanzania imeweza kusisitiza elimu kwa wananwake na wasichana ambapo kwa sasa inajenga shule za serikali katika kata zote nchini.

“Moja ya changamoto zinazowakumba wanawake na kuleta tatizo katika mkataba huu ni kuhakikisha wanawake wanapewa uwezo wa elimu ili waweze kuwa washiriki kamilifu katika maendeleo ya nchi zao, kwa upande wa Tanzania moja ya mambo yaliyosisizitwwa sana ni elimu kwa wasichana na wanawake,”

“Kwa sasa Serikali inahakikisha inajenga shule za sekondari katika kata zake 3956, shule za msingi katika vijiji vyote 12,319 na inatekeleza mpango mpya wa boost wa kuboresha elimu msingi na pia inajenga madarasa 12,000 ya elimu ya awali” amefafanua Prof. Kabudi.

About the author

mzalendo