Uncategorized

WAKILI HELLAR: ZINGATIENI SHERIA, KANUNI, MIONGOZO NA MAADILI KWENYE UTOAJI HUDUMA ZA AFYA

Written by mzalendo

Watoa huduma wameaswa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na miiko ya maadili wanapotoa huduma kwa wananchi kwani Sekta ya Afya inaoongozwa na nyenzo hizo ili kumlinda mtoa huduma na anayehudumiwa.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Wakili Veronica Hellar wakati akiwasilisha mada isemayo “Masuala ya Kisheria na Kimaadili katika Huduma za Afya” kwenye kongamano (symposium) linalofanyika kila wiki kwa watoa huduma wa MNH na kuongeza kuwa kutokutunza siri, kutokuandika kwa ufasaha taarifa za mgonjwa kwenye mfumo, kutokuzingatia kupata idhini ya mgonjwa kwa baadhi ya huduma na uzembe wa aina mbalimbali kunaleta athari kwa hospitali, mtoa huduma na mgonjwa.

Wakili Hellar amesisitiza matibabu ya mgonjwa ni siri ambayo mtoa huduma hapaswi kumpa hata mwenza au ndugu bila ridhaa ya mgonjwa.

“Watoa huduma za afya wana wajibu wa kisheria na kimaadili wa kutunza siri za wagonjwa, ambayo ni moja ya haki za kikatiba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya 1, Sehemu ya 3, (Haki za Msingi) 16 (1)”, amesema Wakili Hellar.

Amesema kuna taarifa ambazo zinaweza kutolewa ikiwemo kwenye elimu na tafiti lakini bila kuonesha utambuzi wa mhusika. Kwa upande wa masuala ya kiuchunguzi wa sababu za kifo au majeraha katika kesi za kijinai, zinaweza kutolewa kwenye mamlaka zenye dhamana hizo ikiwemo jeshi la Polisi na Mahakama.

Kwa upande wa idhini (consent), amewakumbusha kutokufanya kazi kwa mazoea na kuzingatia kupata idhini ya mgonjwa katika baadhi ya vipimo au huduma na idhini hiyo iwe ya kimaandishi isipokuwa kwa huduma za dharura kwa mtu ambaye hajitambui kwa wakati huo.

Amewasisitiza kuendelea kuandika kwa ufasaha na ukamilifu taarifa na mwenendo wa matibabu ya mgonjwa kila hatua ili pale zinapohitajika zipatikanane kwa ukamilifu wake.

Amewahimiza kendelea kuboresha mawasiliano kila wakati kati ya mtoa huduma na mpokea huduma kwani ni haki ya mgonjwa na pia mgonjwa anayo haki ya kukubali au kukataa matibabu fulani.

Kuhusu suala la uzembe (medical negligence) Wakili Hellar amesema watoa huduma wanapaswa kuziepuka kwa kutimiza wajibu au kutoa huduma kwa kuzingatia taratibu na miongozo na kukiuka ni hatari kwa mgonjwa, hospitali na mtoa huduma husika.

About the author

mzalendo