Featured Kitaifa

ZANZIBAR YAJIPANGA KUFANYA MAGEUZI YA KIELIMU

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Lela  Mohammed  Mussa Akitoa Taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na mageuzi katika sekta ya elimu huko Ofisini kwake Mazizini Mjinin Unguja.

Na Fauzia Mussa ,       Maelezo

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  imekusudia kufanya mageuzi  ya kielimu kwa kuifanya Elimu ya amali kuwa ya lazima baada ya kukamilika kwa marekebisho ya sheria ya elimu ya  mwaka 1982 na sera ya mwaka  2006.

Akizungumza  na waandishi wa habari kuhusu  mabadiliko hayo huko Ofisini kwake Mazizini Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Lela  Mohammed Mussa amesema mabadiliko hayo itasaidia wanafunzi kuwa na ujuzi na maarifa watakapomaliza masomo yao.

Aidha alisema hatua hiyo inafanyika kufuatia mabadiliko ya mtaala wa elimu ya maandalizi na msingi ulioanza kutumika mwaka huu wenye  lengo la kuwafanya wanafunzi wanaomaliza  kidato cha pili kuendelea na elimu yao katika madarasa ya amali.

Vilevile Wizara  inakusudia kufuta mitihani ya Taifa ya Darasa la nne na la kumi baada ya kuona matokeo mazuri ya utekelezaji wa mtaala mpya wa ujenzi wa umahiri.

Waziri lela amesema Wizara inakusudia kuweka  miundombinu ya TEHAMA katika Skuli zote ili kuwezesha maendeleo ya kidijitali na kuimarisha Tehama na ubunifu katika elimu pamoja na kuanzisha program za ufundi za TEHAMA ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa  kompyuta,simu  za mkononi pamoja na biashara ya mitandao ya kijamii.

Alifahamisha kuwa katika kuboresha mazingira ya elimu Wizara inakusudia kuanzisha dahalia za michepuo katika Wilaya zote ambazo zitapelekea mchanganyiko wa wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali  na kuimarisha usawa wa utoaji wa huduma za elimu.

 

About the author

mzalendoeditor