Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Lela Mohammed Mussa Akitoa Taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na mageuzi katika sekta ya elimu huko Ofisini kwake Mazizini Mjinin Unguja.
Na Fauzia Mussa , Maelezo
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imekusudia kufanya mageuzi ya kielimu kwa kuifanya Elimu ya amali kuwa ya lazima baada ya kukamilika kwa marekebisho ya sheria ya elimu ya mwaka 1982 na sera ya mwaka 2006.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mabadiliko hayo huko Ofisini kwake Mazizini Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Lela Mohammed Mussa amesema mabadiliko hayo itasaidia wanafunzi kuwa na ujuzi na maarifa watakapomaliza masomo yao.
Aidha alisema hatua hiyo inafanyika kufuatia mabadiliko ya mtaala wa elimu ya maandalizi na msingi ulioanza kutumika mwaka huu wenye lengo la kuwafanya wanafunzi wanaomaliza kidato cha pili kuendelea na elimu yao katika madarasa ya amali.
Vilevile Wizara inakusudia kufuta mitihani ya Taifa ya Darasa la nne na la kumi baada ya kuona matokeo mazuri ya utekelezaji wa mtaala mpya wa ujenzi wa umahiri.
Waziri lela amesema Wizara inakusudia kuweka miundombinu ya TEHAMA katika Skuli zote ili kuwezesha maendeleo ya kidijitali na kuimarisha Tehama na ubunifu katika elimu pamoja na kuanzisha program za ufundi za TEHAMA ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa kompyuta,simu za mkononi pamoja na biashara ya mitandao ya kijamii.
Alifahamisha kuwa katika kuboresha mazingira ya elimu Wizara inakusudia kuanzisha dahalia za michepuo katika Wilaya zote ambazo zitapelekea mchanganyiko wa wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali na kuimarisha usawa wa utoaji wa huduma za elimu.