Burudani Featured

WAZIRI NDUMBARO AAGIZA BASATA NA BODI YA FILAMU KUSIMAMIA SEKTA YA SANAA  KUKUZA UCHUMI WA NCHI

Written by mzalendoeditor

Na Shamimu Nyaki

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameliagiza Baraza la Sanaa la Taifa na Bodi ya Filamu nchini kuhakikisha zinasimamia vyema Sekta ya Sanaa iweze kuchangia katika  ukuaji wa uchumi wa nchi na kunufaisha wasanii.

Dkt. Ndumbaro ametoa maagizo hayo Oktoba 17, 2023 wakati wa hafla ya kukabidhi Tuzo za Hollywood and African Prestigious Awards (HAPAWards) 2023 walizoshinda Wasanii kutoka Tanzania, Jacob Steven aliyeshinda kipengele  cha Best Bongo Movie Actor na Saraphina Michael ( Phina) aliyeshinda kipengele cha Best  Female in Bongo  Fleva East Africa zilizofanyika hivi karibuni nchini Marekani.

“Rais Dkt. Samia ameendelea kufanya juhudi ili Sekta hii ikue, hivi karibuni katika ziara yake nchini India ameshuhudia Utiaji Saini wa Mkataba wa ushirikiano kati ya Tanzania na India katika Sekta ya Utamaduni na Sanaa, na tayari tumepokea maombi ya ushirikiano na Uturuki na Urusi. Hivyo jukumu letu ni kuhakikisha wasanii wetu wanatengeneza kazi zitakazoleta Ushindani Duniani” amesema Dkt. Ndumbaro.

Ameiagiza Ofisi ya Hakimiliki nchini (COSOSTA) ihamikishe inasimamia Sheria ya CMO’S kikamilifu ili wasanii wanufaike na kazi zao, huku akiwaagiza wasanii kutengeneza kazi zenye ubora zinazotangaza utamaduni na lugha ya Kiswahili.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA Dkt. Kedmon Mapana amesema Tuzo hizo zimeanzishwa na Mtanzania anayeishi Marekani Mawinny Casey  ambapo hadi sasa zimefanyika kwa miaka Saba mfululizo zikijikita katika Burudani na Filamu.

Naye Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Dkt. Kiagho Kilonzo ameeleza kuwa katika ziara yao nchini Marekani pamoja na kupokea Tuzo za Wasanii hao pia walishiriki Majukwaa mbalimbali ya biashara, kukutana na wawekezaji wa Sekta hizo na kukubaliana kushirikiana katika kuanzisha Shule ya Filamu,  uzalishaji na usambazaji wa filamu, kazi za kitamaduni pamoja na ujenzi wa jumba changamani la Filamu.

Wasanii wengine  kutoka Tanzania ambao waliwahi kushinda Tuzo hizo ni Wema Sepetu na Lady Jaydee ambao Tuzo zao zimeshafika nchini tayari kwa kukabidhiwa.

About the author

mzalendoeditor