Featured Kitaifa

WATOTO 45 KUFANYIWA UPASUAJI WA MOYO

Written by mzalendoeditor

Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids la nchini Marekani wakimfanyia mtoto upasuaji wa kuziba tundu lililopo kwenye moyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano iliyoanza leo. Jumla ya watoto 45 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi hiyo

Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Mendingi Kids la nchini Marekani wakimfanyia mtoto upasuaji wa tundu dogo kuziba tundu lililopo kwenye moyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano iliyoanza leo. Jumla ya watoto 45 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi hiyo

Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Mendingi Kids la nchini Marekani wakiandaa vifaa vitakavyotumika kwenye upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab kwa mtoto ambaye mishipa yake ya damu imebana wakati wa kambi  maalumu ya siku tano ya matibabu ya moyo kwa watoto iliyoanza leo. Jumla ya watoto 45 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi hiyo

Picha na: JKCI

Na: Mwandishi Maalumu – JKCI

Watoto 45 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yakiwemo matundu kwenye moyo, na matatizo ya mishipa ya damu kufanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalum inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids lililopo nchini Marekani.

Kambi hiyo maalumu ya siku tano ilianza jana na kutoa matibabu ya upasuaji wa moyo wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab kwa watoto 25 na upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua kwa watoto 20.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela alisema upande wa cathlab watoto 25 watapatiwa matibabu ya kuziba matundu mbalimbali yaliyopo katika kuta za moyo pamoja na kufungua mishipa ya damu iliyobana inayopeleka damu kwenye mapafu na kwenye mwili.

Dkt. Stella alisema kupitia kambi mbalimbali zinazofanyika JKCI zimekuwa zikitoa fursa kwa madaktari wazawa kuendeleza ujuzi wao kwani wamekuwa wakikutana na mabingwa waliofanya kazi kwa muda mrefu hivyo kuongeza ujuzi zaidi.

“Kambi ya wataalamu wa afya kutoka Shirika la Mending Kids ni moja ya kambi inayotupa nafasa wataalamu wa JKCI kujifunza mbinu mbalimbali za kutoa huduma bora za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto”, alisema Dkt. Stella

Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Felix Shonyela alisema Idara ya upasaji mkubwa wa moyo imepanga kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto kati ya watatu hadi wanne kila siku wakati wa kambi hiyo maalumu.

Dkt. Shonyela alisema wakati wa kambi maalumu watafanya upasuaji wa moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yakiwemo matundu katika moyo na mishipa ya damu ambayo haiko sawa inayopeleka damu kwenye mapafu.

“Katika kambi hii tutaenda kurekebisha mishipa ya damu ambayo haiko sawa inayoelekea kwenye mapafu na kupelekea mishipa mingine inayochukua damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye mapafu kuwa midogo, tunarekebisha mishipa hiyo ili damu iweze kwenda vizuri kwenye mapafu”, alisema Dkt. Shonyela

Dkt. Shonyela alisema watoto ambao mishipa yao ya damu haiko sawa mara nyingi wakiwa wanafanya michezo huchoka kwasababu hakuna mbadilishano mzuri wa hewa ya oksijeni katika mapafu kwasababu damu inayokwenda katika mapafu inakuwa kidogo.

Naye mzazi ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi hiyo kutoka Mkoani Tanga Herieth Mbelwa alisema wazazi wengi wamekuwa wakiogopa kusikia watoto wao wanaumwa magonjwa makubwa kama ilivyo magonjwa ya moyo hivyo kuacha kuwapeleka Hospitali na kuwatibu kwa miti shamba.

Herieth alisema mtoto wake ana miaka minne na amekuwa akitibiwa shida ya nimomia hadi mwaka huu alipoamua kufika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na mtoto kugundulika kuwa na tundu kwenye moyo.

“Naamini kupitia kambi hii baada ya upasuaji ambao mtoto wangu kafanyiwa jana utaenda kuondoa changamoto alizokuwa akipitia kama za ukuaji, kutokuongezeka uzito, kuchoka na kushindwa kucheza”, alisema Herieth

Kambi hiyo iliyoanza jana tayari imeshatoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto saba ambapo watoto watatu wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo na watoto wanne wamefanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab.

About the author

mzalendoeditor