Featured Kitaifa

MTATURU ALIA NA KIVUKO BARABARA IKUGHA

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ametembelea eneo linalotarajiwa kujengwa kivuko cha muda ili kuondoa hatari inayopatikana kwa wanafunzi katika kipindi cha mvua wanaokatiza mto Matengia uliopo kati ya Kitongoji cha Ighuka na Ikugha jimboni humo.

Mtaturu katika ziara hiyo ameambatana na Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA),Wilaya ya Ikungi Mhandisi Alli Mimbi na wamekagua eneo linapokatiza mto ili kufanya tathimini ya kuweka kivuko na hivyo kuondoa changamoto inayojitokeza wakati wa masika inayosababisha wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo.

Akizungumza katika eneo hilo Mtaturu amesema wao wanawajibu wa kuhudumia wananchi.

“Nafahamu hapa kuna watu wameshakufa kutokana na kukosekana na kivuko hapa,sasa nia yangu tuangalie mpango wa dharura ili tupate ufumbuzi na watu waweze kuvuka,”.amesema.

“Hizi ni jitihada zangu binafsi,najua upo mpango wa muda mrefu huo uendelee, lakini kwa sasa tuwe na utatuzi wa muda mfupi,sitaki kuja kuona mwakani tena narudi naambiwa jambo lile lile ambalo tulishaliongea mwaka uliopita, hapana mimi hamu yangu ilikuwa mwaka wa fedha uliopita tuonane tuweze kuangalia lakini hatukuweza kufanya hivyo,”ameongeza.

Mtaturu amesema jitihada zinazofanywa za kuwa na suluhisho la kudumu ziendelee wakati wanaangalia mpango wa muda mfupi ili kuwanusuru wananchi hasa watoto wanaotumia njia hiyo.

“Mwisho wa siku uhai wa mwananchi ni muhimu na uchumi wao ni muhimu kwa hiyo lazima vyote viwili vifanyike ili kuondoa hofu kwa wazazi juu ya usalama wa watoto wao pindi mvua inaponyesha,”amesema.

Amesema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imepeleka huduma kila mahali ambapo huduma mojawapio ni mawasiliano ya barabara hivyo yeye kama mbunge ni lazima asaidiane na serikali ili ufumbuzi upatikane.

“Hapa nahitaji nipate suluhisho la muda mfupi ,kwa hiyo mhandisi pamoja na mipango ya muda mrefu uliyoniambia mimi nipo tayari twende pale tukapige hesabu tujue kama mimi naweza nikatafuta saruji,nondo na wananchi wakaleta mawe,kokoto na mchanga angalau tupitishe hata kalavati la midomo miwili chini juu watu wapiti,mimi nipo tayari kusaidia hilo,”amesisitiza.

“Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Tawi na Mwenyekiti wa kitongoji nendeni mkawaambie wananchi mimi nipo tayari hivyo nianze kuona mmesogeza mawe ,nianze kuona mnasogeza mchanga kabla mvua haijaja ili ikija hata kama mawe mengi yakibaki sio tatizo,nyie onyesheni nia kama ipo,”ameongeza.

Kwa upande wake Mhandisi Mimbi amesema wameangalia eneo hilo wameona ardhi yake ni nzuri ina asili ya mwamba hivyo inafaa kujengwa kivuko cha muda.

“Sasa kuna mahesabu huwa tunafanya lakini mahesabu tuliyofanya mwaka jana hayawezi kuwa sawa na mwaka huu hivyo ni lazima tukae tuweke hesabu sawa na hilo tutalifanya,”amesema.

Nae Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Tawi la Ikughaa Japhet Kiemi amesema changamoto wanayopata watoto wakati wa mvua ni kubwa .

“Hapa mvua ikinyesha inaweza hata wiki ikapita watoto hawajaenda shule na hivyo kupelekea watoto kutosoma sawa sawa hivyo hili daraja likijengwa litakuwa na faida sana kwetu,tunakushukuru Mbunge wetu kwa moyo wako wak uendelea kuona shida zetu na kuzitatua,”amesema.

About the author

mzalendoeditor