Featured Kitaifa

PROF. JANABI: MCHANGO WA SERIKALI UTOAJI HUDUMA ZA FIGO NI MKUBWA

Written by mzalendoeditor

Serikali imeweka mchango mkubwa katika utoaji huduma za matibabu kwa wagonjwa wa figo katika ngazi mbalimbali nchini kuanzia kwenye kusomesha watalaamu, miundombinu na mashine za usafishaji damu hadi upandikizaji.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Prof. Mohamed Janabi alipokutana na wagonjwa wanaosafishwa figo na ndugu zao ili kujadiliana nao changamoto mbalimbali wanazokutana nazo ili kutafuta ufumbuzi kwa pamoja.

Amesema Uongozi wa Hospitali umepokea maoni yao na kuahidi kufanyia kazi changamoto zilizobainishwa ili kuboresha zaidi hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa hao.

Prof. Janabi amesema MNH-Upanga ina jumla ya wagonjwa 367 wanaosafishwa figo ambapo kati yao 190 wanatumia bima, 163 ni wagonjwa wa kuchangia huduma ambao wanapaswa kuchangia TZS. 180,000 ila kutokana na changamoto za kifedha wengi wao wanalipa viwango tofauti ambavyo ni kati ya TZS. 150,000, TZS. 50,000 na wengine wanatibiwa kwa njia ya msamaha hivyo Serikali inafidia kiasi kilichosalia. Seti ya kumsafisha mgonjwa damu (dialysis kit) mwenye tatizo la figo mara moja sokoni inauzwa TZS. 189,500 na inatumika mara moja.

“Ukiacha tu malipo, bado Serikali kwa MNH ilinunua na kusimika mashine 53 toleo la kisasa namba 5,008 ambapo 42 zipo Upanga na 11 Mloganzila”, amesisitiza Prof. Janabi.

Prof. Janabi amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanakata bima ya afya kabla hawajaugua na kutunza afya zao ili wasiugue magonjwa yanayoweza kuepukika.

About the author

mzalendoeditor