Featured Kitaifa

WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA WANANCHI WAPONGEZA MABORESHO MUHIMBILI

Written by mzalendoeditor

Wananchi mbalimbali waliofika kupata huduma Hospitali ya Taifa Muhimbili leo, wameupongeza Uongozi wa Hospitali kutokana na maboresho mbalimbali ya utoaji huduma yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika.

Pongezi hizo zimetolewa leo na wananchi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Prof. Mohamed Janabi aliyeongozana na timu ya Menejimenti kutembelea vituo vya kutoa huduma ikiwemo Jengo la Wagonjwa wa Nje linaloona wagonjwa takribani 1,000 kwa siku, Idara ya Radiolojia na maeneo mengine ikiwa ni kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja ambayo mwaka huu inafanyika kuanzia tarehe 2 hadi 6 Oktoba yenye kauli mbiu isemayo TUWAJIBIKE PAMOJA.

Wananchi hao wameeleza kufurahishwa na maboresho mbalimbali ndani ya Hospitali ikiwemo hali ya utoaji huduma za vipimo vya uchunguzi upande wa radiolojia, huduma za wagonjwa wodini pamoja na wagonjwa wa nje.

Prof. Janabi amesema MNH itaendelea kuboresha huduma siku hadi siku ikiwa ni utekelezaji wa vipaumbele vya sekta ya Afya hususani huduma kwa wateja.

“Katika kuboresha huduma kwa wateja tunafanya kwa vitendo na ninyi ni mashahidi kuwa kuanzia lango kuu la Hospitali tumefungua Ofisi ya Maulizo ya kisasa ambayo wananchi wanapata huduma kabla ya kuingia ndani ya Hospitali na hali kadhalika majengo yote ya kutolea huduma yana Maafisa Huduma kwa Wateja” amesisitiza Prof. Janabi.

Amewataka wafanyakazi wa Hospitali hiyo kila mmoja kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza wajibu wake kikamilifu sehemu yake ya kazi, kuuliza mwananchi yoyote anayekutana naye ili kuona kama amehudumiwa na kumwelekeza kwa heshima na lugha ya staha.

Ni rahisi sana kumwelekeza mwananchi kwa lugha ya staha na siyo kwa ukali au kumfokea kwani ukiwa unamwelekeza kwa upole na yeye amekasirika anaweza kupunguza ukali mkaongea na kuelewana vizuri zaidi, ameongeza Prof. Janabi.

Sambamba na hilo, Prof. Janabi amewasihi wananchi kujiunga na bima ya afya kabla ya kuugua ili watakapougua waweze kutibiwa kwa urahisi pamoja na kujenga utamaduni wa kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka.

About the author

mzalendoeditor