Featured Kitaifa

WANANCHI GEITA WACHANGAMKIA UCHUNGUZI WA SARATANI BURE,WANAWAKE WAPEWA NENO

Written by mzalendoeditor

Wananchi waliotembelea Maonesho ya sita ya teknolojia ya  Madini Geita jana wakisubiri katika banda la Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita ili kujiandikisha na kupata huduma za uchunguzi wa saratani na elimu kutoka kwa wataalam wa tiba. Huduma hiyo inayotolewa bila malipo na Hospitali ya Rufaa ya Geita kwa kushirikiana na Kampuni ya Geita Gold Mining Company Limited (GGML), inajumuisha uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, matiti na tezi dume. 

 

Baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni GGML, wakifanyiwa uchunguzi saratani katika banda la Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita.

…………………………. 

Wananchi Geita wachangamkia uchunguzi wa saratani bure, wanawake wapewa neno

– Advertisement –

Ad image

NA MWANDISHI WETU

MAONESHO ya Sita ya Teknolojia ya Madini Geita yameendelea kuwanufaisha wakazi wa Geita na viunga vyake baada ya wananchi na wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali kujitokeza kupata elimu pamoja na kufanyiwa uchunguzi saratani.

Huduma hiyo inayoendelea kutolewa bure na Hospitali ya Rufaa ya mkoa Geita kwa ushirikiano na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), inahusisha upimaji wa satarani ya shingo ya kizazi, matiti na tezi dume.

Hatua hiyo imekuja wakati dunia ikielekea katika mwezi Oktoba ambao ni wa uelimishaji kuhusu saratani ya matiti.

Wakizungumza na mwandishi wetu katika banda linalotoa huduma hizo kwenye Viwanja vya Bombambili -EPZ Mjini Geita, mmoja wa wananchi hao, Neema Mgase ambaye ni mkazi wa Nyamalembo mkoani Geita mbali na kuelezea huduma nzuri alizozipata alishauri wakazi wa mkoa huo wafike kupata huduma hizo hasa ikizingatiwa ni bure.

“Wanawake tunapitia changamoto mbalimbali ikiwamo uzazi na nyingine ndio maana nikaona nije kupata uchunguzi.

“Wito kwa kampuni nyingine ni kusaidia jamii ya watanzania ambao wengi tupo katika hali duni kutokana na umaskini kuwekeza kwenye huduma kama hizi ili kusaidia kuboresha afya kwa jamii,” alisema.

Naye Mzee Masele Athuma ambaye ni mkazi wa Nyantorotoro A, alisema amehamasika kufanya uchunguzi wa saratani ya tezi dume hasa ikizingatiwa yupo kwenye umri ambao anaweza kunyemelewa na magonjwa mbalimbali ikiwamo saratani.

“Wito wangu kwa wakazi wa Geita wajitokeze kwa wingi kujua afya yao kwani ndio afya ndio maisha yako. Kwa kweli GGML tunaishukuru imetusaidia wana Geita, mfano kwa maonesho haya ndio mdhamini mkuu hivyo natoa wito kwa kampuni nyingine ziungane na GGML kwa maendeleo ya wananchi wa Geita.

“Nikiangalia kule Nyankumbu tumejengewa shule bora ya sekondari wasichana na wanasoma bure kwa kweli GGML imetusaidia sana,” alisema.

Hoja ya inaungwa mkono na Paschal Shagembe ambaye pia ni mkazi wa Nyantorotoro ambaye kwa upande wake anasema kilichonisukuma kupima afya ni kwamba sasa  magonjwa ni mengi kwani anaweza kuwa ameathiriwa na saratani lakini hajui.

Kwa upande wao wafanyakazi wanawake wa kampuni ya  GGML nao walifanyiwa uchunguzi wa saratani akiwamo, Muuguzi katika hospitali ya GGML, Chitegetse Rushatsi ambaye alisema ameamua kwenda kupata elimu na kufanya uchunguzi wa saratani kwa sababu anatamani kutembea akiwa anajiamini.

“Kwa sababu saratani haioneshi dalili, kitakachokufanya ujue hauna saratani ni kupima tu, na sio njia nyingine yoyote ndio maana nimeshawishika kwenda kupima nijiamini,” alisema na kuongeza;

“Wito wangu kwa wanawake wapime wajijue afya kwa sababu huwezi kujijua una saratani kwa kutembea tu au kumuangalia mtu. Isipokuwa ni pale utakapoanza kuonesha dalili na ukishaanza kuonesha dalili hapo saratani imefikia hatua ambazo ni ngumu kutibiwa,” alisema.

Naye Happy Ijumba ambaye pia ni mfanyakazi wa GGML alisema alipoisikia fursa hiyo kwamba kuna huduma zinatolewa alikuwa mstari wa mbele kutamani kuja kufanya uchunguzi wa kina kuhusu afya yake.

“Kwa sababu saratani si ugonjwa wa kawaida, na kwa sisi wanawake mpaka upate dalili kuona viashiria ujue tayari umeshakuathiri, ndio maana nikaona umuhimu kuja kupata vipimo kujua kama nimepata hivyo virusi au lah,” alisema na kuongeza;

“Nawasihi wanawake wenzangu waje kupima afya zao, wapime saratani ya shingo ya kizazi na matiti kwani inakuwezesha kujiamini na vipimo ni kila baada ya miaka mitatu,” alisema.

Akizungumzia utoaji wa huduma hizo, Mratibu wa huduma za Tiba katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa Geita, Dk. Pasclates Ijumba alisema wameamua kutoa huduma hizo ili kudhibiti madhara ya saratani hususani kwa wananchi ambao wamekuwa waoga kufanyiwa uchunguzi kutokana na na dhana potofu iliyojengeka ndani ya jamii.

Alitoa mfano kuhusu chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi ambayo hutolewa kwa mabinti wadogo, baadhi ya jamii huwazuia watoto wao kupatiwa chanjo hiyo kutokana na ukosefu sahihi wa elimu kuhusu chanjo hiyo.

About the author

mzalendoeditor