…..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya kupitia kwenye kamati za mapato za wilaya wakutane na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wa Idara ya Mapato kwenye Halmashauri ili kufanya ukaguzi kwenye maeneo ya biashara na kuhakikisha risiti za EFD zinazotumika ni zile zinazotokana mashine zilizothibitishwa na kusajiliwa.
“Ni muhimu kila kiongozi anayehusika ashiriki katika kuhamasisha matumizi ya mashine za EFD na kufuatilia hali ya utoaji wa risiti kwa nidhamu kubwa bila kusababisha usumbufu na kero kwa wafanya biashara.”
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Septemba 30, 2023 ) wakati wa Kilele cha Maonesho ya Juma la Utalii na Uchumi wa Bluu yaliyofanyika wilayani Mafia, Pwani. Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika uwepo wa watu ambao wanajihusisha na biashara ya kuuza risiti za EFD kwa wafanyabiashara au watu walionunua bidhaa bila risiti.
Pia, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iendelee kutoa elimu na kuhamasisha matumizi sahihi ya Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD). ”Ndugu wananchi kila unapokwenda kununua bidhaa yoyote dukani na maeneo mengine hakikisha unapata risiti inayotoka kwenye mashine iliyothibitishwa. Tunaendelea kufanya ukaguzi.”
Waziri Mkuu amesema jambo hilo ni ukiukwaji wa sheria na matakwa ya kufanya biashara nchini, hivyo ameitaka TRA iendelee kusimamia sheria, kanuni na taratibu za nchi na kuhakikisha kila mfanyabiashara anafanya biashara kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kwamba TRA ihakikishe inafuatilia kikamilifu wateja wanapewa na kudai risiti zaEFD kwa nidhamu kubwa bila ya kusababisha usumbufu au kero kwa wafanyabiashara na wateja kwa ujumla.
Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kunakuwa na mazingira rahisi yatakayowawezesha wafanyabiashara wa ndani na nje kufanya biashara zao.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Wilaya nchini waimarishe Mabaraza ya Biashara katika wilaya zao pamoja na kukutana na wafanyabiashara na kusikiliza changamoto zao na ushauri wao ili biashara ziweze kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mkoa wa Pwani na wilaya ya Mafia waweke mikakati ya kuongeza kasi ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo yao ili kuongeza idadi ya watalii.
“Mkoa uweke mkakati wa uwezeshaji wa wananchi wanaofanya shughuli za uchumi wa buluu, Serikali ya Mkoa na Wilaya wasaidieni vijana na wajasiriamali wengine kupata fursa za elimu na mikopo ya kuendesha shughuli za biashara.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Watanzania wajenge utamaduni wa kufanya utalii wa ndani. “Tembeleeni Mafia mjionee uzuri uliopo. Tembeleeni na vivutio vingine, niwahakikishie kuwa gharama kwa wazawa katika vivutio vyetu vya utalii ziko chini ili wananchi waweze kumudu. Wekeni utaratibu wa kutunza akiba mpate fursa ya kutembelea vivutio vilivyopo nchini kwetu.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary Majaliwa wakisalimiana na viongozi wa Mkoa wa Pwani na Wilaya ya Mafia walipowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Mafia ambako Waziri Mkuu alihutubia Kilele cha Maadhimisho ya Juma la Utalii na Uchumi wa Bluu (Mafia Island Festival), Septemba 30, 2023.(Picha na ofisi ya Waziri Mkuui)