Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande ,akizungumza mara baada ya kupokea ripoti ya 17 ya tathmini ya utendaji kwa mwaka wa fedha 2022/23 kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), hafla iliyofanyika leo Septemba 29,2023 jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande ,akipokea ripoti ya 17 ya tathmini ya utendaji kwa mwaka wa fedha 2022/23 kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi hiyo, Dkt. Leonada Mwagike, hafla iliyofanyika leo Septemba 29,2023 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
NAIBU Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande ameziagiza Mamlaka ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kushirikiana na vyombo vingine kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki kwa Taasisi 12 za umma zilizoisababishia Serikali hasara ya shilingi bilioni 8.77.
Mhe.Chande ametoa maagizo hayo leo Septemba 29,2023 jijini Dodoma wakati akipokea ripoti ya 17 ya tathmini ya utendaji kazi ya mwaka wa fedha 2022 – 2023 kutoka Mamlaka ya udhibiti wa manunuzi ya umma (PPRA) kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba.
Mhe. Chande amesema ripoti hiyo imebainisha kuwa Serikali ilipata hasara hiyo kutokana na ukosefu wa uwajibikaji, ufanisi, uwazi na uadilifu katika Taasisi 12 zilizochunguzwa.
Mhe.Chande amesema kuwa vitendo hivyo ni vya jinai vinavyohujumu uchumi wa nchi na hivyo hatua kali hazina budi kuchukuliwa kwa wahusika wote.
“Kwa msingi huu, natoa maelekezo kwa vyombo husika vya jinai ikiwemo TAKUKURU, kuchukua hatua stahiki.
“Aidha ni dhahiri kuwa serikali haitazivumilia hata kidogo taasisi zinazokiuka Sheria, Kanuni na Miongozo ya ununuzi wa umma na hivyo kurudisha nyuma juhudi za kuleta maendeleo zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita”amesisitiza Mhe. Chande
Hata hivyo amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali kusimamia na kulifuatilia kwa karibu ili kuhakikisha taasisi nunuzi zote za Serikali kuzingatia Waraka wa Hazina Na. 2 wa mwaka 2023/24, kwa kuhakikisha zinafanya ununuzi wa umma kupitia mfumo wa NeST kuanzia tarehe 1 Oktoba 2023.
Aidha, ameipongeza PPRA kwa uchunguzi na ukaguzi maalum ulioufanya na kuiwezesha Serikali kuokoa fedha za umma ambazo zitaenda kutumika katika kuleta maendeleo ya nchi na kutoa huduma kwa watanzania kama vile ujenzi wa vituo vya afya na madarasa.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Dkt. Leonada Mwagike amesema Mamlaka hiyo ilifanya ukaguzi kwa Taasisi nunuzi 180 ikihusisha Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Mashirika ya Umma.
Alisema katika matokeo ya ukaguzi huo yanaonesha kuwa kati ya Taasisi 180 zilizokaguliwa Taasisi 28 zilikuwa na matokea ya kuridhisha, 109 zilikuwa na matokeo ya wastani na taasisi 43 zilikuwa na matokeo hafifu.
“Kati ya Taasisi 43 zilizopata matokeo hafifu Taasisi 28 zilikuwa kwenye kundi la Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, 8 zilikuwa kwenye kundi la Mashirika ya Umma na Taasisi 7 zilikuwa kwenye kundi la Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na Wakala wa Serikali”, Alibainisha Dkt. Mwagike.
Zoezi la kukabidhi ripoti hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ambayo inaitaka PPRA ndani ya miezi mitatu baada ya mwaka wa fedha kumalizika kutoa taarifa ya utendajikazi na tathmini utendaji kwa mwaka uliopita.