Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ikindwa (Bukene) Wilayani Nzega mkoani Tabora,(hawapo pichani) wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Mzunguko wa Tatu, Awamu ya Pili katika wilaya hiyo kwa kuwasha umeme katika kijiji hicho na kuzungumza na wananchi.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Ikindwa (Bukene) Wilayani Nzega mkoani Tabora,wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Mzunguko wa Tatu Awamu ya Pili katika wilaya hiyo kwa kuwasha umeme katika kijiji hicho na kuzungumza na wananchi.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Ikindwa (Bukene) Wilayani Nzega mkoani Tabora,wakifurahia kuwashwa kwa umeme katika kijiji hicho na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (wa pili kulia) wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa umeme Vijijini Mzunguko wa Tatu Awamu ya Pili .
Meneja Msimamizi wa Miradi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Romanus Lwena akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ikindwa (Bukene) Wilayani Nzega mkoani Tabora,(hawapo pichani) wakati wa ziara Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Mzunguko wa Tatu Awamu ya Pili katika wilaya hiyo kwa kuwasha umeme katika kijiji hicho na kuzungumza na wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Bukene Suleman Zedi akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ikindwa (Bukene) Wilayani Nzega mkoani Tabora,(hawapo pichani) wakati wa ziara Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini mzunguko wa Tatu Awamu ya Pili katika wilaya hiyo kwa kuwasha umeme katika kijiji hicho na kuzungumza na wananchi .
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga(kulia) akitoa maelekezo kwa mwakilishi wa Mkandarasi anayetekeleza mradi wa usambazaji umeme katika Kijiji Ikindwa (Bukene) Wilayani Nzega mkoani Tabora, wakati wa ziara ya kukagua Maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini mzunguko wa Tatu Awamu ya Pili katika wilaya hiyo kwa kuwasha umeme katika kijiji hicho na kuzungumza na wananchi.
Na Zuena Msuya na Theresia Lugwisha, Tabora
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameweka historia kwa kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika Kijiji cha Ikindwa (Bukene) Wilayani Nzega mkoani Tabora, tangu kuanzishwa kwa kijiji hicho baada ya nchi kupata uhuru.
Kapinga amefanya tukio hilo, tarehe 25 Septemba 2023 katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini mzunguko wa tatu Awamu ya Pili katika wilaya hiyo kwa kuwasha umeme katika kijiji husika na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo.
Akizungumzia mradi huo, Kapinga amesema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza mradi wa usambazaji umeme vijijini katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo vituo vya afya, Taasisi za elimu, Taasisi za Dini, Masoko, Visima vya Maji na Mashamba.
“Niwatoe hofu kuwa wananchi wote mtamfikiwa na umeme, kazi iliyombele yenu ni kusuka waya katika nyumba zenu, ili umeme utakapofika maeneo yenu kazi iwe ni kuwaunganisha tuu tena kwa gharama nafuu ya shilingi 27,000. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo kuwa wananchi wote waunganishiwe umeme” alisema Kapinga.
Aidha ametoa siku saba kwa mkandarasi anaetekeleza mradi huo katika kijiji cha Ikindwa kuwalipa ujira wao vijana waliofanya kazi ya kuchimba mashimo, kusimika nguzo pamoja na kuvuta waya ambao mpaka sasa bado hawajalipwa fedha zao.
Alimueleza mkandarasi huyo kuwa jukumu la kusimamia malipo ya wafanyakazi hao ni la kwake na si la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) hata kama anaweka kampuni za kumsaidia katika kazi hiyo.
Sambamba na hilo aliwataka wakandarasi wote kukamilisha na kukabidhi kazi waliopewa ya kusambaza umeme vijijini ifikapo mwisho wa mwezi Desemba 2023 tena bila visingizo vya aina yeyote ili kumaliza kazi ya kusambaza umeme vijijini na kuhamia katika Vitongoji.
Kapinga amewagiza wakandarasi kufanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa na wafahamu kuwa jukumu la kuwaunganishia wananchi umeme ni la kwao, aidha hakuna mkataba utakaokamilika endapo mkandarasi hatamaliza kuwaunganishia umeme wananchi aliokabidhiwa.
Kwa upande wake Meneja Msimamizi wa Miradi kutoka wakala wa Nishati Vijijini( REA), Mhandisi Romanus Lwena amewataka wananchi kutumia umeme huo kwa shughuli za uzalishaji mali ili kupata maendeleo na kujiongezea kipato.
Vilevile amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ya uwepo wa mkandarasi katika maeneo yao kwa kuandaa nyumba zao ili kuunganishiwa umeme na wasisubiri hadi pale mkandarasi atapoondoka katika maeneo yao.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha kilichowezesha wao kupata umeme tangu kuanzishwa kijiji mara baada ya kupata uhuru.
Wamemuahidi Naibu Waziri wa Nishati Kapinga, kuwa watatekeleza ushauri aliowapa kwa kuandaa nyumba zao ili kukaa tayari kwa kuunganishiwa umeme pindi utakapofika katika maeneo yao.