Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU: SERIKALI KUTUMIA SH. BILIONI 42 MRADI WA MAJI MULEBA

Written by mzalendoeditor

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani humo, Septemba 24, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*Ni za mpango wa Serikali wa kusambaza maji hadi vijijini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kujenga mradi wa maji wa sh. bilioni 42 kwa ajili ya kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria na kuyasambaza kwenye kata sita za wilaya ya Muleba. 

“Kwa kuanzia, Serikali imetoa sh. milioni 800 kwa ajili ya kuyavuta kutoka ziwani, yaje kwenye tenki lililojengwa ili yasafishwe na yatibiwe kisha tuyasambaze kwenda vijijini. Tumeshafanya hivyo kwenye miji ya Tarime, Musoma Vijijini, na sasa tumeanza Bunda, Busega, Magu na Geita. Kote huko tunatoa maji ziwani na kuleta vijijini,” alisema.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana jioni (Jumapili, Septemba 24, 2023) wakati akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Muleba kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Fatuma, wilayani humo. 

Alizitaja kata hizo kuwa ni Kikuku, Bureza, Kagoma, Muleba, Magata, Kikuku na Gwanseli na kuongeza kuwa utafiti ukikamilika utasaidia kubaini ni vijiji vingapi tupeleke maji. “Tunaposema kata, ni pamoja na vijiji vyake vyote.” 

Amesema katika sekta ya maji, mbali na hizo sh. bilioni 42, Februari mwaka huu Serikali ya Dkt. Samia ilitoa sh. bilioni 5.73 kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa maji kwenye wilaya hiyo. Akitoa mchanganuo, Waziri Mkuu alisema: “Mradi wa maji Bulamula ulipewa shilingi milioni 681; Rutenge shilingi milioni 600; Ilemera shilingi milioni 599; Katare shilingi bilioni 2.96 na Kyamiyorwa shilingi bilioni 3.2.”

Wakati huohuo, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wakazi hao wawe wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kuratibu suala la upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na mipakani.

“Kitambulisho cha Taifa ni usalama wa nchi, ni usalama wa Taifa letu; kwa hiyo anayestahili kukipata ni Mtanzania tu. Na kujua Kiswahili siyo Utanzania. Kwa hiyo inabidi tuwe makini na kila mmoja wetu awe mzalendo na lazima tutambuane,” alisisitiza.

Alisema amepokea maoni ya Wabunge wa mkoa huo ya kwamba Serikali ipeleke maofisa wengi zaidi wa Uhamiaji na NIDA ili wafanye uchunguzi wa waombaji na kuwafanyia uhakiki hukohuko.

Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya kikazi mkoani Kagera.

About the author

mzalendoeditor